Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna.
Dar es Salaam, Tanzania - Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna, ametunukiwa tuzo ya heshima ya uongozi bora wa biashara barani Afrika kwa uongozi wake shupavu wa taasisi hiyo kubwa ya fedha kuliko zote nchini Tanzania.
Ruth Zaipuna ametunukiwa tuzo hiyo maalum ya “African Business Leadership Commendation Award” ya mwaka 2022 na jarida la African Leadership kwa juhudi zake za kuifanya Benki ya NMB kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa taifa na kuchangia kikamilifu kuboresha maisha ya Watanzania.
Jarida hilo linaloshapishwa na Taasisi ya African Leadership Organisation yenye makao yake makuu huko London nchini Uingereza, lina ushawishi mkubwa kimataifa na linaheshimika kwa kuyatangaza mafanikio ya bara la Afrika duniani.
Kwa mujibu wa mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa taasisi hiyo, Dkt Ken Giama, sababu zilizofanya Bi Zaipuna kuibuka kidedea ni pamoja na uongozi wake uliotukuka na kuifanya NMB kuwa kinara wa ubunifu kwenye sekta ya benki nchini.
Dkt Giama alisema zaidi ya kuwa kiongozi mahiri na mwenye msimamo thabiti wa kibiashara, pia uongozi wake umechangia sana kusaidia NMB kutengeneza fursa nyingi za ajira na kuzalisha mali nchini na barani Afrika kwa ujumla.
“Umechaguliwa kwa kauli moja kutunukiwa tuzo hii maalum ya uongozi bora wa biashara barani Afrika na uteuzi wako unatokana na umahiri wako wa kuongoza na ubunifu katika sekta ya benki,” Dkt Giami alisema kwenye barua aliyomwandikia Bi Zaipuna kuhusu kutunukiwa kwake tuzo hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa ushindi wa Bi. Zaipuna ulitokana na mchakato makini unaozingatia sifa stahiki uliofanywa na timu ya uteuzi ya bodi ya wahariri wa Taasisi hiyo.
Kiongozi huyo wa NMB alitunukiwa heshima hiyo wakati wa kilele cha mkutano wa maendeleo ya Afrika na Tuzo za Uongozi wa Biashara za Afrika (ABLA) zilizofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa House of Lords katika Bunge la Uingereza.
Akizungumza kabla ya kupokea zawadi ya Bi Zaipuna wakati wa shughuli hiyo, Mkuu wa Idara ya Teknolojia na Mabadiliko ya Kidijitali wa NMB, Bw Kwame Makundi, alisema heshima hiyo ya kimataifa ina maana kubwa sana kwa Benki ya NMB na Tanzania kwa ujumla.
Aliwaambia washiriki wa hafla hiyo kuwa tuzo hiyo ni ushahidi wa juhudi za makusudi ambazo uongozi wa Benki ya NMB umekuwa ukizingatia ili kuboresha maisha ya Watanzania na kusaidia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Bi Zaipuna alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Bw Makundi kuwa tuzo hiyo haitambui tu mafanikio na mchango wake kama kiongozi bali pia unatambua mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita na Benki Kuu ya Tanzania kuiwezesha NMB kustawi na kuendelea kuwanufaisha wadau wake wote.
“Ninashukuru kuwa kiongozi wa taasisi yenye sifa endelevu za kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanayochangia kubadili na kuboresha maisha ya watu wengi. Hili kwangu ni jambo kubwa sana.”
Taarifa kwa umma ya benki hiyo ilisema ushindi wa Bi Zaipuna na washindi wenzake 10 wa tuzo za ABLA za mwaka huu zilizofanyika Julai 10 pia ni matokeo ya umakini wao wa kibiashara na mafanikio makubwa katika maendeleo ya sekta binafsi barani Afrika.
Mkutano wa Afrika ni moja ya programu muhimu za jarida la African Leadership unaowaleta pamoja viongozi wa taasisi za umma na sekta binafsi kutoka Afrika, Ulaya na Marekani kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali kwa ajili ya mustakabli mpya wa bara hili na ulimwengu wote.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana, inaonyesha kuwa mbali na Bi Zaipuna, wengine walioshinda tuzo za ABLA zilizotolewa Julai 4, 2022 ni Mfanyabiashara na Bilionea wa Lesotho Sam Matekane aliyeshinda tuzo ya heshima ya Maisha, Waziri wa Fedha wa Mauritius Dr Renganaden Padayachy, tuzo ya Kiongozi bora wa Biashara Afrika ilienda kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Mitaji Nigeria Dr Akintoye Akindele, Afisa Mtendaji Mkuu wa United Capital Plc ya Nigeria Mr Peter Ashade alishinda Afisa Mtendaji Mkuu wa Mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment