NA TATU MOHAMED
AFISA Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum, Baraka Lucas amesema kutokana na kuwepo kwa mifumo mingi ya utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia imesaidia kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo kufichuliwa.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Habari Mseto katika maonesho ya 46 ya kimataifa ya Biashara (DITF), yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema miaka ya nyuma watu walikuwa hawatoi taarifa za vitendo vya ukatili huo kutokana na mifumo hiyo kutokuwa rafiki pamoja na kutokuwa na elimu ya kutosha.
"Sasa jamii imeelimika na kuweza kubaini mifumo hii na kuweza kuitumia ipasavyo kwa kutoa taarifa dhidi ya vitendo hivyo," amesema Lucas.
Hata hivyo amesema sababu ya vitendo vya ukatili kushamiri ni matokeo ya watu kupata athari mbalimbali ikiwemo mtu ambaye aliwahi kutendewa hivyo kuamua kulipiza na wengine ni kutokana na hali ugumu wa maisha.
"Ukatili unaofanyika unaweza kuwa wa kisaikolojia, kimwili au uchumi na asilimia kubwa ya watu wanaokutana navyo vitendo hivi ni wanawake na watoto kwa sababu kundi hili limekuwa na nafasi ndogo ya kujitetea," amesema Lucas.
Kwa Upande wake Mratibu wa Kitengo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisheria kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) Rufina Khumbe amesema taasisi yao imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inatoa elimu juu ya masuala ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, huduma za afya pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi na watu mbalimbali wanaofika katika kituo chao.
Amesema wamekuwa wakitembelea shule na vyuo mbalimbali pamoja na makanisa katika kutoa elimu hizo mbalimbali kwa kufanya hivyo wamekuwa wakiwafikia watu wengi zaidi.
"Huduma yetu tunayotoa katika vituo vyetu kikiwemo cha Kijitonyama ni bure kabisa na kipo kwaajili ya watu wote sio kwa wanafunzi pekee yao,tumeweza kufika katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha tunawajengea uwezo watu kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi wa mpango ,magonjwa ya Ukimwi pamoja na Magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanaathiri watu wengi kutokana na mpangilio wa chakula," amesema.
Amebainisha kuwa katika maonesho hayo, wanatoa ushauri na nasaha ambapo zaidi ya watu 130 wameweza kufika katika banda lao na kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kupokea ushauri na nasaha.
“Watu ni wengi wanafika katika banda letu na wanajifunza vitu mbalimbali na kupokea ushauri na nasaha miongoni mwa vilivyoonekana kutolewa kwa watu hao ni pamoja na ushauri na nasaha juu ya migogoro ya familia, masuala ya ukatili pamoja naushauri wa hali za msongo wa mawazo," amesema Rufina.
No comments:
Post a Comment