NA TATU MOHAMED
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),imekuja na ingizo jipya la mashine ya kuchakata matunda na viungo kuwa katika mfumo wa unga ili kumsaidia mkulima kuhifadhi mazao yasiharibike kwa muda mrefu.
Akizungumza kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam,katika banda la VETA,mbunifu wa mashine hizo George Nyahende alisema mashine hiyo ni nyenzo bora ya kisasa inayomsaidia mkulima hata mjasiriamali kuchakata mazao na kuyaongezea thamani.
Nyahende amesema mashine hiyo ina sehemu tatu ambazo kila moja ina kazi yake. Moja ni ya kukatakata viungo au matunda tayari kwa kuyakausha kwenye machine nyingine ndogo na baada ya hapo inaingia kwenye mashine ya kusaga kuwa unga.
"Huu ni ubunifu mpya, niliona wakulima hususani vijijini wanapata hasara ya mazao yao mfano vitunguu wanavuna wakati mwingine soko halipo vinaharibika,sasa wakitumia mashine hii wanavikausha vitunguu na kuvisaga kuwa unga na hapo unahifadhi kwa muda mrefu,"amesema Nyahende.
Amesema aliamua kubuni mashine hiyo kwa sababu hivi sasa maeneo mengi ya vijijini umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA),wamesambaza umeme maeneo mengi hivyo wakulima wengi wanaweza kununua mashine hiyo na kuondokana na umaskini.
Amesema seti ya mashine hiyo ni shilingi milioni moja na ina muda wa matazamio kwa mteja wa mwaka mmoja baada ya kuinunua na kusema ina ubora na malighafi zilizotumika kutengeneza zimetoka ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa mashine hiyo sio mtu kwa mkulima bali pia kwa wajasiriamali wadogo wanaweza kufungua kiwanda kidogo nyumbani na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na kukuza uchuni wao.
Amesema vikundi vya wajasiriamali wanaweza kuinunua na kuitumia kuzalisha bidhaa zao kwa kuwa inamatokeo mazuri na yenye viwango vya ubora.
Amesema moja ya mashine hizo ambayo ni ya kukausha matunda,viungo au nyama hutumia muda kati ya saa sita hadi 12 kulingana na bidhaa na baada ya hapo unasaga na kupata unga kisha unaweza kuufungasha kwa ajili ya kuhifadhi.
Amewataka wajasiriamali na wananchi kutembelea banda la VETA katika maonesho hayo kujionea mashine hiyo ili kuelimishwa na kuinunua kwa sababu ina faida nyingi za kuongeza kipato.
No comments:
Post a Comment