Na Mwandishi Wetu
MMOJA
wa Watanzania ambao wamefanya mambo ambayo hayawezi kusahaulika katika
nchi hii ni Abdallah Athuman Seif maarufu Abdallah King Kibadeni Mputa,
ama Ndururu.
Katika
mahojiano aliyofanya na mwandishi wetu hasa yakilenga miaka 45 ya
kipigo kisichosahaulika cha mabao 6- 0 ilichokitoa Simba SC kwa watani
zao Yanga Afrika katika mchezo wa ligi tarehe 19 ya mwezi Julai mwaka
1977, mzee Kibaden aliongelea masuala mbalimbali ya soka na pia akigusia
kuhusu historia yake binafsi.
Anaelezea kuwa jina lake halisi ni Abdallah Athuman Seif na ni mzaramo kwa mama yake mzazi na kwa baba ni mngindo.
Anadai
jina hili la Kibaden lilikuja tu na wala si la kuzaliwa,jina lake
halisi ni Abdallah Athuman Seif na hivyo kufafanua baba yake mzazi ni
marehemu Athuman Seif.
*Jina hili la Kibaden limetokea wapi?*
Alipoulizwa
sababu haswa ya yeye kuitwa Kibaden na badala ya jina lake halisi la
Abdallah Athuman Seif, mzee Kibaden anadai kuwa jina hili alipewa wakati
akiwa anasoma madrasa wakati wa udogo wake vijana wenzake wakati huo
walikuwa wakimuimbia kwa utani kuwa "Abdallah Kibaden,Kanya mavi
Mtendeni,kasingizia wageni" anadai jina hilo ambalo marehemu baba yake
hakupendezewa nalo lakini lilishika kasi na kuzoeleka vinywani mwa watu.
Alhaj
King Kibaden anasema baada ya kuendelea kuzoeleka kwa jina hilo la
Abdallah Kibaden hatimaye jina lake la tatu la Seif nalo likaondoka
baada ya kwenda Songea kuichezea kwa mafanikio klabu ya Maji Maji ya
Songea ambapo akiwa huko licha ya kukaribishwa vizuri na wana "Lizombe"
walimpatia heshima ya kipekee na walimvika jina la machifu waliokuwa
katika vita ya Maji Maji alipatiwa jina la "Mputa" ambaye huyu alikuwa
kiongozi wao wa katika vita ya Maji Maji hatimaye kumfanya sasa
kuzoeleka kwa majina ya Abdallah Kibaden Mputa na kuachana na jina
halisi la Abdallah Athuman Seif,majina haya aliyatambulisha rasmi katika
mamlaka husika kama ndio yatakayotumika kama majina yake halisi.
Alhaj
King Kibaden ambaye ni mmoja wa waumini wa kiislam aliyehudhuria ibada
ya Hijja huko Saudi Arabia na kumfanya aitwe Alhaj anaendelea kusema
kuwa yeye elimu yake ilikuwa mpaka middle school (darasa la nane) na
elimu ya madrasa ya kumtukuza Mwenyezi Mungu. Anadai alipomaliza darasa
la Nane alimuomba baba yake amruhusu aachane na kuendelea kielimu na
badala yake ajikite kwenye soka acheze mpira wa miguu.
Alianza
kucheza soka toka mwaka 1970 alipojiunga na timu ya Kahe Sports Club na
kisha baadae alijiunga na timu kubwa ya wakati huo ya Sunderland
ambayo kwa sasa inatambulika kama Simba SC.
Miaka
nane yake ndani ya uchezaji uliotukuka katika Simba kulihitimishwa
mwaka 1978 alipojiunga na "wana Lizombe" Maji Maji ya Songea. Akiwa
Maji Maji alicheza mpaka mwaka 1984 kwa takriban miaka sita.Licha ya
kuchezea Maji Maji lakini pia kipindi hicho alianza kusomea masomo ya
"football coaching" na kuhitimu mwaka huo huo wa 1984.
Pia amesomea kozi mbalimbali za football coaching Ujerumani, Mauritius, Ubelgiji nk
*Alhaj King Kibaden ana mafanikio yapi anayojivunia nayo?*
Katika
vitu anavyojivunia Alhaj King Kibaden ni kucheza kwa mafanikio katika
Simba SC ambapo aliipa mataji kadhaa na pia kuwa na rekodi
isiyosahaulika ya kufunga magoli matatu kwa mkupuo katika mechi moja ya
watani wa jadi. Rekodi hiyo kwa miaka 45 sasa haijavunjwa na mchezaji
yeyote katika michezo yote ya mashindano yoyote yaliyozikutanisha timu
hizo kubwa Tanzania.
Pia
bado ana rekodi ya kipekee ya kuipeleka Simba SC katika fainali ya
michuano ya CAF ambapo akiwa Kocha mkuu wa timu ya Simba huku akisaidiwa
na kocha toka Ethiopia Antenne Eshete Simba SC ilifikia Fainali ya
kombe la CAF,rekodi ambayo mpaka leo miaka 29 haikuvunjwa na timu yoyote
Tanzania toka kuifikia Simba mwaka huo wa 1993.
Anajivunia
katika kikosi chake cha 1993 licha ya kuvifunga vilabu vikubwa vingi
huku bajeti ikiwa finyu lakini alikuwa na wachezaji wote wazawa wa
Tanzania waliokuwa na moyo na mapenzi ya dhati yaliyochanganyika na
uzalendo kwa timu na taifa lao.
Alhaj King Kibaden pia alifundisha vilabu kadhaa vya ndani na nje ya Tanzania huku akikuza vipaji vya wachezaji wengi Tanzania.
Alhaj
King Kibaden aliwahi kufundisha soka Oman na kwa hapa Tanzania
alivifundisha vilabu vya Mtibwa,Simba,Maji Maji,Kagera Sugar,team za
Taifa Stars na Serengeti Boys ambapo Serengeti Boys licha ya kufaulu
iliondolewa katika mashindano kufuatia mchezaji Nurdin Bakari kuwa na
matatizo ya "registration" yake.
*Ni kipi hasa kilimpa nguvu ya kuifikisha Simba SC katika fainali ya CAF?*
Akijibu
swali hilo mwalimu Alhaj King Kibaden anatanabaisha kuwa maandalizi
yalikuwa mazuri na kwa wakati ule team ilikuwa inasimamiwa kiufadhili
na Mfanyabiashara Azim Dewji na marehemu Privatus Mtemanyenje "Priva
Mtema".
Anadai kulikuwa na kambi Zanzibar ambayo ilikuwa eneo tulivu na wazanzibar walikuwa wakiisapoti kambi kwa kila kitu.
Anasisitiza
kuwa imani kubwa kwa Mwenyezi Mungu iliyowashika kila aliyekuwa katika
team ndio siri kubwa ya wao kufika Fainali ya CAF.
Anachokumbuka ni kuwa kila siku za swala ya Ijumaa yeye alikuwa anaomba kufanywe maombi ya timu kuwa na mafanikio.
Kingine
ni motisha,anakumbuka Mfadhili Azim Dewji alikuwa anawapa motisha
mbalimbali ikiwamo zawadi ya gari kwa kila mchezaji iwapo Simba itatwaa
taji la CAF.Zawadi hiyo ilikuwa ni kutolewa kwa magari aina ya KIA.
Wachezaji walikuwa wanajitambua na kujituma huku yeye akiwapa elimu ya uzalendo wa taifa lao.
Alhaj King Kibaden ama kwa hakika ni nguli na mwenye kuufahamu mpira wa Tanzania na Afrika.
Anashauri
klabu yake ya Simba inaweza kumtumia akatoa mchango wake kwa kuwa bado
uwezo huo anao hata wa kuwa katika ushauri kwa wachezaji na benchi la
ufundi.
Kwa sasa
anamiliki academy yake ya soka inayofahamika kama Kibaden International
Soccer Academy (KISA) iliyopo Chanika,Dar Es Salaam.
Kituo
kinaendelea kuzalisha wachezaji wengi wazuri ambao wanapelekwa katika
vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu na Ligi daraja la Kwanza.
Vipi kuhusu wao wachezaji wa zamani wanapewa heshima ama ushirikiano na klabu ya Simba kwa sasa?
Akijibu swali hilo Mwalimu Alhaj Kibaden anadai wanakosa ushirikiano na bila ya kuelewa sababu haswa ni nini.
Anashauri klabu iwe inawathamini wachezaji walioitetea klabu kwa kila nia na njia mpaka imepata mafanikio hapo ilipo.
*Vipi kuhusu usajili?*
Mwalimu
Alhaj King Kibaden ametanabaisha kuwa kiutaalam hawezi kulijibu kwa
kuwa mpira unachezwa kutokana na jinsi mwalimu anavyofundisha,sasa
hafahamu uwezo wa Mwalimu na hata hawa wachezaji.Tofauti na zamani
ambapo ulikuwa unaweza kujua uwezo wa mwalimu au mchezaji.
Ana
imani kwa benchi na uongozi kuwa wanaelewa nini hasa wana Simba
wanahitaji kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa,hivyo
wanaweza kufanya usajili mzuri ili waonekane kuwa wamefanya kazi nzuri
na kutimiza ahadi kwa wanachama,wapenzi na mashabiki wa SSC.
Ana
imani wachezaji hawa wa sasa watajitahidi kwa kuzingatia kuwa sasa
mpira ni ajira na wanapata sifa na pesa,hivyo si rahisi kama watafanya
utovu wa nidhamu na kuwaharibia performance.
No comments:
Post a Comment