WAZIRI wa Nishati January Makamba ameeleza kuwa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limejipanga katika kuboresha huduma na kurahisisha upatikanaji na usambazaji wa umeme kwa gharama nafuu nchi nzima.
Aidha Waziri Makamba amesema Tanzania ni mahala sahihi pa uwekezaji kwani pana mazingira bora na wenzeshi ya uwekezaji ikiwemo huduma wezeshi za umeme, nishati ya gesi pamoja na mafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda la TANESCO katika maonesho ya 46 ya kimataifa ya biashara maarufu kama Sabasaba Makamba amesema kuwa, amefarijika na mwenendo wa shirika hilo kwani limekuwa zaidi ya kiufundi na uhandisi.
“Mwelekeo wa kihuduma unaonekana, mambo mazuri yanakuja ndani ya miaka miwili, mitatu ijayo litakuwa shirika bora na lenye viwango bora la utoaji huduma, mambo ya shirika hili yanakwenda sambamba na bajeti ya wizara tuliyoitoa bungeni kwa maslahi ya watanzania wote,” ”amesema Makamba na kuongeza
”Tukiwa kama wizara, Serikali na taasisi ni jukumu letu kuhakikisha mawasiliano kwa umma ni muhimu ili wananchi waweze kuelewa ni nini tunafanya na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha huduma zinazotolewa na wizara pamoja na taasisi zake.” amesema.
Makamba amesema amefarijika baada ya taasisi hizo na viongozi wake kushiriki kwa ukaribu zaidi na kuwahudumia wananchi katika maonesho hayo kwa ukamilifu akiwemo Mkuregenzi mkuu wa TANESCO Maharage Chande.
”Tunaona namna suala hili lilivyo muhimu kwa Wizara na taasisi zote, mawasiliano, elimu na huduma kwa Umma ni muhimu kwetu tunamwona MD Chande yupo hapa akishiriki kutoa huduma kwa wananchi hii ni namna ambayo tumejipanga katika kuhakikisha kila mwananchi anapata na kufikiwa na huduma kwa kiwango bora zaidi.” ameeleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Maharage Chande amesema kuna miradi mingi ya kuhakikisha wanazalisha umeme wa kutosha na alama za uzalishaji ziwe himilivu.
”Tuna miradi mingi ya kuhakikisha nishati ya umeme inakuwa ya uhakika ikiwemo mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere utakaotumia maji na mingine itakayotumia gesi, tunaamini kupitia miradi hii tutakuwa na umeme wa kutosha, bei himilivu na tutakuwa washindani katika ukanda wa Afrika.” amesema.
Chande amesema shirika hilo lenye mitambo ya umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1700 ina miradi ya umeme ya kuunganisha Tanzania na nchi nyingine katika Ukanda wa Afrika ikiwemo Kenya, Zambia na Msumbiji na uwepo wa gesi ya kutosha nchini itasaidia kuzalisha umeme mkubwa na kuweza kufanya biashara ya umeme kwa kushirikiana na nchi za ukanda.
No comments:
Post a Comment