NA TATU MOHAMED
WAZIRI
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amezitaka
taasisi za Serikali kutumia teknolojia ya TEHAMA ya kuendesha mikutano
kwa njia ya mtandao (video conference).
Aidha
Waziri Nape amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa
hatua madhubuti zinazochukuliwa katika kuhakikisha huduma ya TEHAMA
inaunganishwa katika ofisi za Serikali na taasisi zake.
Nape
amebainisha hayo alipotembelea Banda la Shirika la TTCL kwenye Maonesho
ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Uwanja wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar es Salaam.
Nape
amesema matumizi hayo ya TEHAMA yatasaidia kiasi kikubwa kupunguza
gharama za Serikali huku hatua hiyo pia ikirahisisha mawasiliano kwa
shughuli za Serikali na watumishi wake.
“Serikali ipo tayari kuwawezesha kutekeleza mpango huo wa TEHAMA, endelee kufanya kazi nzuri ya kuwahudumia watanzania,” amesema
Akiwa
katika Banda hilo la TTCL amepata fursa ya kuona huduma mbalimbali
zinazotolewa na shirika hilo ikiwemo huduma ya Faiba Mlangoni kwako,
iliyowavutia zaidi wadau wa mawasiliano nchini.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema
shirika hilo limejipanga kuhakikisha linaziunganisha taasisi na ofisi za
Serikali katika matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha shughuli zote za
Serikali ikiwemo mikutano.
Amesema
TTCL ndiyo mtoa huduma wa kwanza kutekeleza agizo la Serikali la
kutumia ‘video comference’ katika mikutano yake na kwamba lengo la
Serikali kutaka kutumia huduma hii ni kupunguza gharama na kuwakutanisha
watumishi kwa njia ya haraka zaidi.
Amesema
mpaka sasa TTCL imeshawaunganisha wateja zaidi ya 10 mkoani Dodoma
ambao wanaendelea kufurahia huduma baada ya kufungiwa mfumo huo.
Akizungumzia
huduma ya Faiba Mlangoni, Mhandisi Ulanga amebainisha kuwa huduma hiyo
ina umuhimu mkubwa kwa mteja kwani itamwongezea uwezo wa kutumia
intaneti kwa haraka na ubora zaidi hivyo kuwashauri wateja kuitumia ili
kufurahia mawasiliano rahisi.
Ameongeza
kuwa huduma ya Faiba Mlangoni inaingia Sokoni kwa lengo la kubadili
soko zima la matumizi ya TEHAMA kwa kuboresha zaidi.
No comments:
Post a Comment