HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 04, 2022

VETA yajipanga kuzalisha nguvukazi



NA TATU MOHAMED 


MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) amesema wamejipanga  kuzalisha nguvu kazi ambayo itawasaidia wawekezaji na wafanyabiashara watakaokuja nchini kufanya shughuli zao.

Amesema nguvukazi inayozalishwa inatosha kutumika katika utalii, viwanda, biashara, teknolojia, ubunifu, madini na gesi.

Maduki ameyasema hayo wakati akikagua bunifu mbalimbali katika banda la VETA ndani ya maonyesho ya 46 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba.

"Mbali na nguvukazi pia tunajitahidi kuzalisha teknolojia ambazo zitatumiwa na wawekezaji ili kuhakikisha wanazalisha katika ufanisi na ubora wa kimataifa na nchi inavyotaka.

"Pia tunavyo vifaa vinavyotumika vinavyoweza kutumiwa na wawekezaji katika uzalishaji au kuongeza uzalishaji," amesema Maduki.

Ameongeza kuwa ili kufanikisha hilo pia wamejipanga kuongeza idadi ya vijana watakaopata mafunzo ya ufundi huku akieleza kuwa vyuo 29 vinamaliziwa katika ngazi ya wilaya na vinne katika ngazi ya mkoa.

"Lengo letu ni kutaka kufikia vijana 700,000 ndani ya miaka mitano wapitie katika vyuo vyetu na kujipatia ujuzi wa aina mbalimbali," amesema Maduki.

Amesema vijana hao watapitia mfumo wa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi na kupatiwa vyeti vyao.

"Na katika hao 700,000 hatutegemei waajiriwe bali wengine wajiajiri na kuzalisha ajira pia waweze kusaidia wawekezaji watakaokuja nchini," amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Antony Kasore amesema wanazalisha nguvu kazi kulingana na sekta za kimkakati.
"Tunafundisha vijana namna ua kufanya kazi migodini, katika gesi ili waweze kuwa msaada," amesema Kasore.

No comments:

Post a Comment

Pages