HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2022

Prof Mbarawa: Serikali inaendelea kufanya maboresho Bandari Meli kubwa ziingie



 Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
 
 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
 

Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imesema inaendelea kusimamia bandari za mwambao na maziwa makuu kwa kufanya maboresho ikiwemo kuongeza kina kikubwa ili kuweza kuruhusu Meli za Kisasa kuingia na kushusha mizigo.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema lengo la kufanya uboreshaji wa bandari hizo ni kusaidia meli kubwa za kisasa ziweze kuingia na sio kwenda kwenye bandari za nchi za jirani.

Amebainisha kuwa vipaumbele vya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2022/23 vinakusudia kuhuisha uchumi wa nchi na kuwakomboa Watanzania wa ngazi zote.

Amesisitiza kuwa kuhusu upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kwamba ujenzi wa gati namba 8 hadi 11 unaenda sambamba na upanuzi wa gati namba 1-2 katika Bandari ya Tanga ili kuziwezesha bandari hizo kufanya kazi kwa ufanisi.

‘Serikali pia itaendelea na upanuzi wa Bandariza Dar es Salaam na Tanga, Ujenzi wa Meli katika Ziwa Victoria na Tanganyika, upanuzi wa viwanja vya ndege nchini na ujenzi wa nyumba za viongozi na  watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini’amesema Waziri Prof Mbarawa

Mbali na hilo kuhusu maendeleo ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) sehemu ya kwanza inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro (Km 300) Prof. Mbarawa amesema kuwa majaribio ya reli hiyo yanatarajiwa kuanza Mwezi Septemba, mwaka huu.

 Profesa Mbarawa amevitaja  vipaumbele vya Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23  huku  vingine ni Ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa km 3.2 Jijini Mwanza, kukamilisha Daraja la Wami linalounganisha Mkoa wa Pwani na Tanga, na Ujenzi wa Barabara za kupunguza msongamano na Magari yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam na barabara za mzunguko mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Pages