HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

October 16, 2026

Rais TOC ateta na waandaaji, aibariki Heavy Weight Plus Size Marathon

NA MWANDISHI WETU


RAIS wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Anthony Mtaka, amezibariki na kupongeza wazo bunifu lililozaa Mbio Maalum za Watu Wenye Uzito Mkubwa ‘Heavy Weight Plus Size Marathon,’ zinazotarajiwa kufanyika Desemba 27 mwaka jijini Dar es Salaam.

Mtaka, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, ametoa pongezi hizo alipokutana na kuzungumza na waandaaji wa mbio hizo Kampuni ya Heavy Weight Sports Promotion na kusema yeye kama muumini wa ubunifu, amevutiwa na wazo hilo na kuwatakia maandalizi mema.

Heavy Weight Plus Size Marathon 2026 zimezinduliwa Oktoba 12 na Mwakilishi wa West Coast Shotokan Karate Association Africa, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa West Coast Shotokan Karate Tanzania, Renshi Taifa Liwewa, ambaye pia alisifu wazo la kuwakutanisha watu wenye uzito mkubwa.

Akizungumza na waandaji hao, Mtaka alisema: “Hongereni sana kwa ujio wenu huu, nawapongeza kwa ubunifu mkubwa uliozaa mbio zenu. Mimi ni muumini wa ubunifu katika utendaji, kwahiyo niliposikia uzinduzi wenu, nikajikuta navutiwa na nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwatakia maandalizi mema.”

Mtaka aliongeza ya kwamba Watu Wenye Uzito Mkubwa ni miongoni mwa makundi yanayopaswa kupewa nafasi ya kushiriki na kushindana michezoni, ndio maana anaamini Heavy Weight Plus Size Marathon ni wazo linaloenda kuchochea jamii kutowabagua watu wanene na wao kutojitenga na michezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Heavy Weight Sports Promotion, Tullo Chambo, alimshukuru Rais wa TOC kwa kubariki mbio zao hizo, ambazo zinashirikisha pia wakimbiaji wasio na uzito mkubwa, wadau wa michezo, wadau wa afya, watoto, taasisi na mashirika.

Chambo na Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo walimtakia Mtaka utekelezaji mwema wa majukumu yake ndani ya TOC alikoingia madarakani katikati ya mwaka huu na kwamba wao kama wadau wa michezo wako tayari kumpa ushirikiano katika kusukuma mbele gurudumu la Michezo ya Olimpiki Tanzania.

Aidha, Uongozi wa Heavy Weight ulimkabidhi Mtaka ‘tracksuit’ rasmi za michezo, ambazo huenda akazitumia atakaposhiriki mbio hizo zitazokimbiwa katika Kilomita 15 (15KM Run), Kilomita 10 (10KM Run), Kilomita 5 (5KM Run/Walk), Kilomita 2 na Nusu kwa Watoto (2.5KM Kids Run) na Fun Run Fitness Jog and Walk.


 

No comments:

Post a Comment

Pages