Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona akizungumza wakati wa kupokea matokeo ya utafiti wa mabaki ya mkonge.
Mtafiti Dk. Aziza Konyo akizungumzia matokeo ya utabiri huo kwa waandishi wa habari.
Mwandishi Wetu, Tanga
UTAFITI umethibitisha kwamba mabaki ya mkonge yanaweza
kuwa chakula cha mifugo chenye protini nyingi, mbolea hai
na nishati.
Matokeo ya utafiti huo yanafungua fursa za kiuchumi na kupunguza changamoto za utunzaji wa mazingira hapa nchini.
Kwa mujibu wa Mtafiti Dk. Aziza Konyo, mabaki ya mkonge huchukuliwa kuwa taka za viwandani zisizo na thamani kwa miaka mingi hivyo utafiti huo ulilenga kutafuta njia mbadala za kutumia mabaki ya mkonge yanayozalishwa kwa wingi ili yatumike kwa manufaa.
"Katika uzalishaji wa nyuzi za mkonge, takribani asilimia nne hadi sita ya malighafi inayogeuzwa kuwa nyuzi nyeupe, huku sehemu kubwa iliyobaki ikihitaji kutafutiwa matumizi yenye tija
badala ya kuendelea kuwa taka.
“Kwenye utafiti wangu nililenga kutatua tatizo la uzalishaji wa taka nyingi katika viwanda vya mkonge kwa kutumia mabaki hayo kuzalisha chakula cha mifugo chenye protini nyingi na mbolea isiyo na kemikali za viwandani,” alisema Dk. Konyo.
Alifafanua kuwa katika kutekeleza utafiti huo, watafiti walitumia teknolojia ya nzi aina ya Black Soldier Fly ambao mabuu yake hulishwa mabaki ya mkonge na kuvunwa baada ya siku 14 hadi 18.
Alisema mabuu hayo hukusanywa, kukaushwa na kutumika kama kiungo cha chakula cha mifugo chenye protini nyingi na mabaki hutumika kutengeneza mbolea hai.
Dk. Konyo alisema baada ya vipimo vya maabara ilionesha kwamba mbolea hiyo inaweza kurejesha rutuba ya udongo na kuongeza virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mimea vikiwemo nitrojeni, fosforasi na potasiamu (NPK).
Kwa upande wake, Mtafiti kiongozi wa mradi huo kutoka Chuo cha Nelson Mandela, Profesa Anthony Mshandete alisema, utafiti huo ni sehemu ya juhudi za kutafuta matumizi yenye tija kwa mabaki ya mazao ya kilimo yakiwemo mkonge na kahawa, kupitia teknolojia ya kuongeza thamani.
Alisema mradi huo unahusisha Tanzania, Kenya, Ethiopia na Denmark ukiwa na lengo la kuchunguza namna mabaki ya mazao yanavyoweza kutumika kuzalisha bidhaa nyingine na kuchangia maendeleo ya kilimo na viwanda.
Profesa Mshandete alisema watafiti pia wanachunguza uwezekano wa kuzalisha nishati kutokana na mabaki ya mkonge yanapochanganywa na mabaki mengine ya kilimo na kuboresha teknolojia zitakazowezesha uzalishaji huo kufanyika kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona alisema bodi hiyo inaendelea kushirikiana na watafiti kutafuta njia mbadala za kuongeza thamani ya mkonge na kuhakikisha mabaki yanayotokana na uchakataji wake yanakuwa sehemu ya fursa mpya za kiuchumi katika sekta hiyo.
“Matokeo ya tafiti zinazolenga kuongeza thamani ya mkonge ni muhimu katika kutafuta matumizi mapya ya zao hilo ili sekta iweze kunufaika zaidi na bidhaa zinazozalishwa na mabaki ya mkonge,” alisema Kambona.






No comments:
Post a Comment