Baadhi ya wananchi wakipata huduma mbalimbali ndani ya Banda la TTCL kwenye Maonesho ya Wakulima Kitaifa Nanenane Mkoani Mbeya. |
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetwaa ushindi wa pili kwa Kundi la Kampuni za Mawasiliano Kitaifa katika kilele cha Maonesho na Sherehe ya Nanenane yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
TTCL imetangazwa mshindi leo katika kilele cha sherehe hizo za maonesho ya Nanenane huku nafasi ya mshindi wa pili kitaifa ikichukuliwa na kampuni ya Simu ya Halotel Tanzania.
Akizungumza katika Banda la TTCL, Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Mujuni Kiyaruzi, amewashukuru Watanzania waliopata fursa ya kuwatembelea katika Banda la TTCL kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu Viwanja vya John Mwakangale na wateja wote wanaoendelea kuwaunga mkono.
Amesema Shirika la Mawasiliano Tanzania limedhamiria kumsaidia mkulima, kuendesha kilimo biashara kwa manufaa hasa kupata taarifa sahihi za masoko kupitia sekta ya mawasiliano ili ziweze kusaidia kupata masoko na hatimaye kukuza kilimo nchini.
"Mwaka huu 2022 tupotena kwenye viwanja vya John Mwakangale Maonesho ya Nanenane sisi TTCL kwa ajili ya kuwafikia wananchi, lakini kwa sababu hizi ni Siku Kuu za Wakulima tumewalenga hasa wakulima na kauli mbiu ya mwaka huu ajenda 1030 kilimo ni biashara na tunapozungumzia biashara hakuna namna utazungumzia biashara bila kuzungumzia uchumi wa kidijitali.
Na sisi kama shirika kubwa la mawasiliano tunawaunganisha wakulima na masoko lakini pia na taarifa zinazohusu mahitaji yao ya kilimo yalioko duniani kwa njia ya mawasiliano ya mtandao na mawasiliano ya simu," alisema Mhandisi Kiyaruzi.
Naye Afisa Mauzo TTCL Mkoa wa Mbeya, Bi. Ida Yesaya alisema wananchi wataofanikiwa kutembelea banda hilo watapata huduma zote kama vile huduma ya mihamala kupitia simu (T-Pesa), huduma za simu za mezani zisizotumia waya, huduma za simu za mkononi na huduma za vifurushi vyote vya simu vya kampuni ya TTCL.
No comments:
Post a Comment