HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 08, 2022

Vijana waaswa kuwekeza kwenye mkonge


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Mariam Nkumbi akizungumza na waandishi wa habari katika banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Mariam Nkumbi akizungumza na waandishi wa habari katika banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Mariam Nkumbi akiangalia bidhaa mbalimbali zinatokana na zao la mkonge katika banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, George Seni na kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge wa TSB, Olivo Mtung'e. 

 

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

 

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Mariam Nkumbi amewaasa vijana kujitokeza katika banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya katika Viwanja vya John Mwakangale ili kujifunza kilimo cha mkonge.
 
Amesema ametoa wito huo kwa vijana kwani kilimo ni njia pekee ya kuwawezesha na kuwainua na zao mojawapo ni kuwekeza kwenye kilimo cha mkonge.
 
Amesema vijana wakipata eneo wakawekeza watafanikiwa kuvuna kwa miaka 15 mfululizo ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka kutembelea kwenye banda la Bodi ya Mkonge Tanzania ili kupata elimu zaidi na kujionea fursa mbalimbali zitokanazo na mkonge.
 
“Kijana acha kuzubaa njoo uwekeze kwenye kilimo, pia wazazi na wazee wote, nawasihi kuwekeza kwenye mkonge ni kumuwekea mtoto wako hazina ambapo ataendelea kuvuna maisha yake yote.
 
“Kwa sasa bodi inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha uzalishaji wa zao la mkonge ambalo kwa miaka ya nyuma lilishuka sana kwa hiyo sasa hivi uhamasishaji mkubwa ni kuendeleza zao la mkonge ndiyo maana tuko kwenye maonyesho ya Nanenane.
 
“Katika banda letu, utapata elimu ya kutosha kuhusu wapi unaweza kupata maeneo ya kulima, nini mnaweza kufanya ili kuendeleza maeneo yenu kwa kilimo cha zao la mkonge,” amesema.
 
Aidha, amesema kwa sasa benki nyingi zinatoa mikopo na mkonge ni miongoni mwa mazao ambayo yanaangaliwa ambapo ameendelea kuwasisitiza vijana kupita kwenye banda hilo kupata elimu ya kutosha na kisha wapite kwenye mabenki wapate elimu kuhusu mikopo ya kilimo ambapo kwa sasa wameshusha riba hadi asilimia tisa.
 
“Kijana acha kuzubaa njoo uwekeze kwenye kilimo, pia wazazi na wazee wote, nawasihi kuwekeza kwenye mkonge ni kumuwekea mtoto wako hazina ambapo ataendelea kuvuna maisha yake yote,” amesema Nkumbi.
 
Aidha, amesema Bodi ya Mkonge iko kwenye mpango wa kufungua ofisi katika kanda zote ambazo zinalima mkonge na kwa kuanzia wameshajiandaa kufungua Ofisi ya Kanda Kilosa kwa ajili ya Kanda ya Kati ili kuwahudumia kwa karibu zaidi wakulima na wadau wa mkonge kwa sababu si lazima watu waje Tanga tu.
 
Pamoja na mambo mengine, amewashauri wanaotaka kulima mkonge kutembelee Kituo cha Utafiti wa Mkonge Mlingano kilichopo Tanga ili kupata elimu zaidi ya nini cha kufanya ili ulime kilimo bora cha mkonge kwa sababu wao ndiyo wazalishaji wakuu wa mbegu za mkonge.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge wa Bodi ya Mkonge, Olivo Mtung’e amesema mkonge una matumizi mengi ambapo kwa sasa wanahamasisha kuongeza uzalishaji zaidi kwani soko ni kubwa na mahitaji ya bidhaa zake ni makubwa.
 
“Lengo letu ni kufikisha tani 125,000 mwaka 2025 ambapo hata kama tutakuwa hatujatosheleza soko lakini angalau tutakuwa tumefikia kiwango kikubwa cha kutosheleza soko na kuwasambazia nyuzi wateja wetu wa nchi za nje.

No comments:

Post a Comment

Pages