Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee wa ACT Wazalendo, Yasin Mohammed Gumsan akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa kushiriki Sensa ya Watu na Makazi. kushoto ni Afisa habari wa chama hicho, Arodia Peter.
Na Mwandishi Wetu
NGOME ya Wazee ACT-Wazalendo wamewataka wazee nchini kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kuanza kufanyika Agosti 23 mwaka huu ili kuweza kuisadia Serikali kulisaidia kundi hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee wa chama hicho, Yasin Gumsan alisema wazee nchini wanatakiwa kuunga mkono zoezi hilo bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa kwakuwa ni suala muhimu hususan katika kupanga mipango ya maendeleo.
“Sisi Ngome ya Wazee tunawakumbusha wazee wote nchi nzima bila kujali itikadi zao za kisiasa kujitokeza kwa wingi siku ya kuhesabiwa, binafsi mimi nikiwa Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee nipo tayari kuhesabiwa.
“Aidha umuhimu wa Sensa tumeuona kwakuwa sisi wazee tunahitaji mambo mengi ambayo tunadhani Serikali yetu haina budi kuyatekeleza, lakini bila kama hatutahesabiwa Serikali haitaweza kutusaidia kwa sababu itakuwa haijui idadi yetu halisi nchi nzima,”alisema Gumsan.
Aidha kiongozi huyo wa wazee wa ACT-Wazalendo alisema Sensa ni muhimu kwakuwa chama chao kinajiendesha kisayansi hivyo kinahitaji kutumia zaidi taarifa za utafiti na takwimu ili pamoja na mambo mengine kujiwekea malengo ya kisiasa.
“Kwakuwa wazee wa Zanzibar hulipwa Sh 20,000 kila mwezi, Tanzania Bara hali ni tofauti kabisa kwani hakuna hata mzee mmoja nje na wale wastaafu ambaye anapatiwa hata glasi moja ya maziwa, hivyo tungependa utaratibu kama huo pia utumike na huku Tanzania Bara”alisema Gumsan.
No comments:
Post a Comment