Waziri wa Maji Jumaa Aweso (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa wa ujenzi wa ofisi ya maabara ya bodi ya maji Bonde la Kati, mjini Singida leo Julai, 30, 2022. Kutoka kulia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, Afisa wa Bodi ya Maji Bonde la Kati, Mhandisi Danford Samson, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru na Mjumbe wa Siasa Mkoa wa Singida, Diana Chilolo.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso (kushoto) akikagua ujenzi wa mradi wa maji, Dareda, Singu, Sigino na Bagara unaotekelezwa Mkoa wa Manyara ambao utagharimu Sh.12 Bilioni.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso,amezindua jengo la ofisi kuu ya Bonde la Kati
zilizopo mjini Singida na maabara za ubora wa maji na kuyataka mabonde mengine
kwenda kujifunza utendaji mzuri wa kazi unaofanya na viongozi wa bonde hilo.
Akizungumza leo Julai 30, 2022 mara baada ya kuzindua jengo hilo ambalo
ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh.bilioni 2.9 hadi kukamilika kwake, alisema
Bonde la Maji Kati litakuwa kama chuo kwa mabonde mengine kwenda kujifunza
kutokana na jinsi wanavyofanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Aweso alisema Wizara ya Maji ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na maji
ya kutosha
hivyo Bodi za Maji nchini ziache kuweka bei za kuwakandamiza watumiaji wa
maji ili wapate nguvu za kuendelea kutunza vyanzo vya maji.
Aidha, alisema baada ya kukamilika kwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi
kukamilika, mabonde yote tisa ya maji nchini yarejewe takwimu za upatikanaji wa
maji nchini.
Aweso alisema Bodi za Maji zihakikishe zinawatambua na kuwashirikisha
watumiaji wa maji kwani wapo baadhi wanatumia maji bila kuwa na vibari lakini
hawatambuliwi.
"Moja ya changamoto ya mabonde yetu yanatumika tu kwa ajili ya
'ambush' tu, washirikisheni, watambuweni wadau wenu wa maji na msiweke bei za
kuwakandamiza, wekeni bei rafiki," alisema.
Aweso alisema wakurugenzi na maafisa wa mabonde ya maji watambue wajibu wao
kwa kutoka maofisini kutoa elimu sahihi ya juu uanzishwaji wa mabonde ya maji.
"Wakati mwingine anapoambiwa mtu kuna taasisi ya bonde anajua pengine
ni kimlima kidogo kidogo, maafisa wa bonde mtoke muwaelimishe wananchi,"
alisema.
Aweso alisema haiwezekani unajiita afisa bonde halafu hata vyanzo vya maji
huvijui na hata watu wanapokuwa na changamoto ya maji hauna ufumbuzi wa tatizo
hilo.
Alisema zifanyike jitihada za kuongeza rasilimali za maji kwani haiwezekani
mvua zinanyesha halafu maji yote yanapotea kwenye bahari.
Waziri Aweso alisema ni muda mwafaka rasilimali za maji kwa maana ya mvua
isiwe kama laana bali iwe baraka na fursa kwa maji ya mvua kuvunwa kwa kujenga
mabwawa ya kimkakati ili maji hayo yatumike kwa matumizi ya kunywa.
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Dk.George Lugomela alisema Bodi ya Maji
Bonde la Kati iliyomaliza muda wake imejitahidi kufanya kazi ambapo imeongeza
ukusanyaji wa mapato kutoka Sh.Milioni 300 zilizokiwa zikikusanywa awali na
kufikia Sh.mil.800.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Pakas Mlagiri, alisema
Bonde ndio injini ya maji sababu wao ndio wanaovisimamia vyanzo vyote vya maji.
Alisema kutokana na umuhimu huo wa mabonde ya maji, kufanyike utafiti wa
kuainisha vyanzo vyote vya maji kuanzia ngazi ya kijijjj na kata kufanya hivyo
kutasaidia upatikanaji mkubwa wa maji.
Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, alisema upatikanaji wa maji
katika manispaa hiyo umefikia kiwango za asilimia 80.
Kiaratu alishauri Bonde la Maji Kati kwa kushirikiana na Halmashauri ya
Manispaa ya Singida kutunga sheria ndogo kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Kati, William Mabula alisema
wamejipanga kufanya vizuri zaidi kwa kusimamia rasilimali za maji na kuongeza
mapato kutoka Sh.milioni 800 hadi kufikia Sh. Bilioni 1.
No comments:
Post a Comment