Na Godwin Myovela, Singida
KAULI Mbiu inayovuma kwa kasi ya Shirika
la Posta nchini (TPC) isemayo ‘Posta Twenzetu Kidijitali-Haijawahi Tokea!
imezidi kujidhihirisha kupitia ofisi za shirika hilo mkoani hapa, ambapo kupitia
wiki ya huduma kwa wateja, mamia ya wananchi wameonyeshwa kufurahishwa na
maboresho ya kihuduma yanayoendelea kutolewa kwa sasa.
Akizungumza
muda mfupi baada ya wafanyakazi wa shirika hilo kushiriki zoezi la kufanya
usafi wa mazingira na kutoa faraja kwa wagonjwa ndani ya hospitali ya mkoa wa
Singida-kama azma yake kwenye ushiriki wa majukumu ya kijamii, Meneja wa Posta
mkoani hapa, Michael Mwanachuo, pamoja na mambo mengine alisema mwaka huu
shirika hilo limekuja kivingine.
Alisema wakiwa kwenye maadhimisho ya wiki
ya huduma kwa wateja, inayokwenda sambamba na shamrashamra za shirika hilo kuelekea
kilele cha siku ya Posta Duniani ambayo huadhimishwa ifikapo Oktoba 9 kila
mwaka shirika kwa kuzingatia mifumo ya kasi ya TEHAMA linaendelea kusafirisha
barua kwa njia ya haraka (EMS) ndani na nje ya nchi na usafirishaji mizigo
mikubwa.
Pia kwa kutumia TEHAMA ya Posta Kiganjani
ambayo humwezesha mteja yeyote kupata huduma za posta popote, Mwanachuo alisema
mpaka sasa fursa mbalimbali kwa matokeo bora na ya uhakika zinaendelea kutolewa
kwa kuzingatia kasi na ufanisi, ikilinganishwa na siku za nyuma.
“Posta kwa sasa tupo kidijitali zaidi
nitoe wito kwa umma kuzidi kutembelea ofisi za shirika letu na kutuunga mkono
kwa kujipatia huduma zetu mbalimbali za kidijitali zilizoboreshwa.” Alisema
Mwanachuo.
Shirika hilo kwa sasa pamoja na mambo
mengine linatoa huduma za kidijitali za Uwakala wa Fedha, Masanduku ya Barua,
Duka Mtandao, Intaneti Café, na mfumo madhubuti wa kufuatilia barua au
kifurushi kilichotumwa kupitia mtandao kujua kimefikia wapi au kimepokelewa na
nani.
Huduma nyingine ni pamoja ‘Posta Cash’,
Uwakala wa Bima, Huduma za uuzaji wa hisa za makampuni mbalimbali na huduma za
Bodi ya Mikopo na Baraza la Mitihani sanjari na huduma kwa wananchi wanaohitaji vyeti vya
kuzaliwa ambapo kazi ya kujaza fomu na nyaraka zote ni sehemu ya majukumu ya
shirika hilo ambapo mwananchi akikamilisha taratibu zote anakwenda kwa Wakala
wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa hatua ya mwisho ya kuchukua cheti.
Shamrashamra hizo zilipambwa na shughuli mbalimbali kwa shirika hilo mkoani hapa kufanya usafi wa mazingira, utoaji wa huduma za kidijitali sanjari na kujumuika kukata na kula keki na wateja wake ‘wakiwemo wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Singida Big Stars’ kama sehemu ya kurudisha shukrani.
No comments:
Post a Comment