Na Sabiha Keis, Zanzibar
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Rahma Kassim Ali, amesema asilimia 80% ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar yanasababishwa na baadhi ya madalali kwenda kinyume na taratibu za kisheria zilizowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari uliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo Maisara jana, Alisema asilimia kubwa ya migogoro ya
ardhi inachangiwa na madalali kwa kuuza viwanja bila kufuata taratibu za kisheria
zilizowekwa katika uuzaji na ununuzi hali ambayo inasababisha migogoro ya ardhi
kuendele kujitokeza nchini.
Alisema kutokana hali hiyo wizara yake inajipanga kuandaa utaratibu maalum wa kuweza kudhibiti tatizo hilo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo. Lakini kuanzia sasa mtu akijulikana anauza kiwanja kinyume na utaratibu sheria itachuka mkondo wake.
"Napenda kuwasihi wananchi wanapotaka kununua ardhi katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kufika katika taasisi husika iliyowekwa kisheria ili kuepusha migogoro ya ardhi kuongezeka Zanzibar"Alisema Waziri Rahma.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na wageni ambao wanania ya kuekeza kufika taasisi husika na kuacha kuwatumia madalali katika hatua za ununuzi wa ardhi kwani umiliki wa ardhi unahitaji hatua mbali mbali za kisheria zikamilike ndipo mnunuzi atakuwa salama katika uwekezaji wake.
Sambamba na hayo Waziri huyo aliwataka wananchi ambao wamepewa viwanja na SMZ kwaajili ya matumizi mbali mbali kuayaendeleza maeneo hayo ili kuzidhibiti kwa lengo la kuepusha uvamizi na kusababisha migogoro ardhi kuendelea kujitokeza kila siku.
Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa agizo la muda wa miezi sita kwa mwananchi aliyepewa ardhi kuendeleza matumizi ya ardhi katika eneo alilopewa mara tu anapopata umiliki rasmi huku raia wa kigeni wamepewa muda wa mwaka mmoja kinyume na hilo eneo hilo litarudi Serikalini.
"Niwatake wananchi pamoja na raia wa kigeni kuhakikisha wanayaendeleza maeneo kwa mujibu wa sheria iliyowekwa na wasipo yaendeleza kwa muda uliowekwa maeneo hayo yatarudi Serikalini" Alisisitiza Waziri Rahma.
Wakati huo huo alifahamisha kua katika kukabiliana na changamoto ya upangaji miji hivi karibuni Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar ilitiliana saini na kampuni ya Properties lnternational kutoka Tanzania bara kwa lengo la kushirikiana katika suala zima la upangaji miji na vijiji ambapo kwa hatua ya awali kazi hiyo itahusisha maeneo ya akiba yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mkutano huo kwa waandishi wa habari umekuja mara baada ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar kufanya ziara katika maeneo mbali mbali pamoja na kufanya tathmini ya ongezeko la migogoro ya ardhi nchini.
No comments:
Post a Comment