HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 31, 2023

TRA yawakumbusha Watanzania kutoa Taarifa za Magendo, yahimiza Maafisa wake kujiendeleza Kielimu

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imewataka Watanzania kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona kuna vitendo vya udanganyifu (magendo) vinavyofanyika hasa katika Maeneo ya Fukwe za Bahari,bandarini kwenye fukwe za Maziwa pamoja na Mipakani.

 


Aidha, mamlaka hiyo imewataka maafisa wake kujiendeleza kielimu kwa kutumia fursa masomo zilizopo kwenye Chuo cha Kodi cha TRA ili kujiimarisha kiutendaji pamoja na kuiongezea nchi mapato. 

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka hiyo, Dinah Edward akimwakilisha Kamishna Mkuu wa Forodha wa TRA, Alphayo Kidata wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha Duniani ambayo hufanyika Januari 26 kila mwaka ambayo imefanyika jijini Dar es Salaam leo. 

Amesema kuwa wananchi wakishiriki kikamilifu kutoa taarifa hizo kutasaidia kupunguza matukio hayo na kuisaidia TRA kuweza kukusanya ushuru na kodi za Serikali.

" Wananchi waendelee kutoa taarifa wanapoona watu wanaofanya vitendo vya magendo na udanganyifu wakifanya hivyo watatusaidia kukusanya mapato ya Serikali," amesema Dinah.

Amesema kuwa TRA imekuwa ikijikita katika kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi hivyo kukwepa kodi ni kinyume cha sheria na kanuni za Serikali.

Pia amesema siku hiyo imewekwa kwa ajili ya kuwaweka pamoja wanachama wa Wakala Wa Forodha ili kuangalia kwa pamoja fursa zilizopo duniani pamoja na kuona namna ambavyo mataifa mbalimbali yanafanya shughuli kwa uwiano sawa.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amewahimiza mawakala wa forodha nchini kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na miongozo, sheria na kanuni za kidunia za taaluma hiyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Forodha wa TRA, Said Athman amesema katika kutekeleza mkataba wa kimataifa wa Wakala wa forodha tayari serikali imeanza kunufaika na biashara za kimataifa pamoja na kukuza pato la Taifa kupitia kodi.

Akizungumzia kuhusiana huduma mbalimbali zinazotolewa na TRA, amesemema kuwa Mamlaka hiyo ni nambari moja kwenye ubunifu, Automation na ufuatiliaji.

“Tumeimprove njia za ukusanyaji Mapato katika vituo mbalimbali vinavyotolewa huduma na TRA ikiwa na huduma za kijamii, Sisi wakala wa Forodha umetupatia Access za kuingia kwenye mifumo na kufanya Return Assessment.” Ameeleza

Nae, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Nchini, Edward Urio, ameiomba TRA kuwashirikisha walipa kodi katika utekelezaji wa mujukumu yao ili kuondoa kodi kinzani kwa wazalisha wa bidhaa mbalimbali.

Shirikisho la Wakala wa Forodha Duniani lilianzishwa mwaka 1952 Nchini Ubelgiji, Tanzania ilijiunga mwaka 1964 lengo ni kujiweka katika nafasi za kimataifa ili kunufaika na misaada pamoja na mafunzo, misaada, ushirikishwaji, pamoja na vikao vinavyofanyika kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Pages