HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2023

CCM ZANZIBAR YAKEMEA VITENDO VYA UKWEPAJI WA KODI

 


 
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis, akionyesha kitabu cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.

 

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema hakitowavumilia baadhi ya watu wanaokwepa kulipa kodi kwa makusudi na kuisababishia hasara kubwa serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis katika mahojiano maalum huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar.

Amesema kila mwananchi ana jukumu la kupinga vitendo vya ukwepaji wa kodi kwani ni hujuma,usaliti na jinai katika maendeleo na ustawi wa uchumi wa nchi.

Mbeto, alieleza kuwa madhara ya vitendo hivyo ni makubwa kwani yanaikosesha serikakali fedha nyingi ambazo zingetumika katika kutatua kero na changamoto za wananchi.

“ CCM ikiwa ndio msimamizi mkuu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 lazima tukemee vikali baadhi ya tabia ya ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya wafanyabishara na wawekezaji.

Fedha hizi zingetumika kujenga hospitali,maskuli,maji safi na salama na huduma za barabara za kiwango cha lami na huduma zingine muhimu za kijamii.”,.alifafanua Mbeto.

Katika maelezo yake Katibu huyo Mbeto, alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, anafanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo endelevu lakini kuna baadhi ya watu wachache wanakwamisha juhudi hizo kupitia vitendo vya ukwepaji wa kodi.

Pamoja na hayo alizitaka taasisi zinazohusika na usimamizi wa masuala ya kodi nchini zikiwemo ZRA,TRA na manispaa  pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanachukua hatua kali kwa yeyote anayehusika na vitendo hivyo bila kujali cheo,dini,kabila na itikadi ya kisiasa.

Sambamba na hayo aliwasihi wafanyabishara nchini  kuwa hakuna haki bila wajibu hivyo ukusanyaji wa kodi ni lazima, kwani ikilipwa wanaijengea serikali uwezo wa kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Alisema serikali zote mbili ya Zanzibar nay a Jamhuri ya muungano wa Tanzania zimetoa fursa kwa wananchi kufuata taratibu za kisheria pale wanapoamua kufanya biashara.

Alifafanua kuwa Ibara ya 47 hadi 49 za Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 imeeleza kuwa CCM inatambua kuwa biashara ni kichocheo cha maendeleo ya viwanda na sekta nyingine za kijamii.

Alisema katika Ilani hiyo ya CCM imeelekeza namna ya serikali itakavyokuza uchumi wa nchi kupitia sekta za biashara na uwekezaji sambamba na kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi.

Kupitia mahojiamo hayo Mbeto, alitoa wito kwa wananchi kuepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kukwepa kulipa kodi huku wakiendelea kuwa wazalendo,wachapakazi na waadilifu.

Aidha, akizungumzia changamoto ya mfumuko wa bei kwa Zanzibar alisema ulikuwa asilimia 7.8 na asilimia 8.1 kwa mwezi Novemba na Desemba 2022, ukilinganishwa na lengo la asilimia 5 ambapo mfumuko huo ulikuwa mdogo kuliko nchi nyingi wanachama wa EAC na SADC kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kupunguza athari za ongezeko la bei za bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi .

Katika hatua nyingine Mbeto, amefafanua kuwa Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuthibiti suala la mfumuko wa bei kwa kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha.

No comments:

Post a Comment

Pages