HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 01, 2023

Migogoro ya Ardhi Zanzibar inasababishwa na wananchi kutofuata sheria

 

Na Sabiha Keis

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Rahma Kassim Ali amesema ongezeko la migogoro ya Ardhi nchini linasababishwa na baadhi ya wananchi kununua Ardhi kwa kutofuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2022 kwa kamati ya Mawasiliano,Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi huko katika ukumbi wa Wizara hiyo Maisara, Unguja.


“Asilimia 80 ya migogoro ya Ardhi inatokana na mauziano ya wananchi kuuziana ardhi kinyume na sheria, na hao wanasheria ndio balaa, kiwanja kimoja kinauzwa mara mbili hata tatu, afadhali hata masheha wakihusishwa wajua kama kiwanja hichi kimeshauzwa “ Alisema Waziri Rahma.

Alieleza kwamba mbali na ununuzi huo wa Ardhi usifuata sheria lakini pia ujenzi holela usiozingatia mipaka halisi ya eneo husika umekua ukichangia kuwepo kwa migogoro hiyo ambapo Wizara yake imejipanga kwa sasa katika kudhibiti hali hiyo.

Waziri Rahma alisema Wizara ya Ardhi tayari imeshakaa vikao mbalimbali na Taasisi zinahusiana  na wizara yake katika masuala ya Ardhi ikiwemo Tawala za Mikoa, Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA) pamoja na Wizara ya Kilimo na kutoka na azimio kuwa vibali vyote vya ujenzi vitolewa katika ofisi moja ili  kuondoa  changamoto iliyopo.

Aidha waziri huyo alisema taasisi yake ya Mahakama ya Ardhi imepokea kesi mpya za migogoro ya ardhi  108 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 ambapo kesi 107 zilitolewa maamuzi huku kesi 183 zinaendelea katika Mahakama hiyo. Kesi hizo ni kwa Unguja na Pemba.


Akizungumzia mikakati ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Mngereza Mzee Miraji amefahamisha kwamba licha ya wizara hiyo kukabiliwa na  changamoto ya fedha lakini wamejipanga kutafuta washirika wa maendeleo kwajili ya  kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo upimaji wa ardhi, kujenga nyumba za bei nafuu na usalama wa ardhi.

“Kwanza tulikuwa na jukumu la kuwa indentify partners, kuangalia jinsi ya kujenga nyumba za low cost, land tenure security pamoja na kuangalia tuanzie wapi? ”Alisema Dkt Mngereza.

Aidha Dkt Mngereza amefahamisha kuwa katika kutatua changamoto ya ujenzi holela Wizara yake tayari imeshatiliana saini na Kampuni ya Propertie International kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya kushirikiana katika kazi ya kupima na kupanga mji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati  Yahya Rashid Abdalla ameipongeza Wizara hiyo kwa namna inavyofanya kazi zake pamoja na kuishauri Wizara  kuhakikisha matumizi ya Ardhi yanalingana  na mahitaji husika.

Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2022 ilikadiriwa kukusanya jumla ya TZS Billioni 1.168 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ndani ya Taasisi zake ambapo hadi kufikia Disemba,2022 jumla ya TZS Millioni 700.550 zimekusanywa ambazo ni wastani wa asilimia 60 ya makadirio.

Kwa upande wa matumizi kwa kipindi Julai- Disemba 2022, Wizara ilipangwa kutumia jumla ya TZS Billioni 2.956 kwa ajili ya kazi za kawaida Na mishahara ambapo hadi kufikia Disemba 2022 Wizara imepatiwa jumla ya TZS Billioni 2.718 ambazo ni wastani wa asilimia 91.9 ya fedha zilizopangwa.

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages