Waziri wa Biashara na
Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaban (katikati), akipata
maelezo kutoka
kwa Meneja Mkazi wa Pesapal, Bupe Mwakalundwa (wa pili kulia) jinsi ya kufanya
malipo kupitia mfumo wa Pesapal badala ya fedha taslimu wakati wa
kongamano
lililowakutanisha wadau wa sekta ya utalii Mjini Zanzibar.
Kushoto ni Meneja Biashara Pesapal, Abdul Hatibu Mwamba na wa pili
kushoto ni Meneja Biashara Pesapal Zanzibar, Sufii Yussufu. Kulia ni Meneja
Mkuu wa Pesapal, Emmy Rono. (NA MPIGA
PICHA WETU).
Na Mwandishi Wetu
Kampuni kinara wa huduma za malipo ya Pesapal imewataka
wadau wa shughuli za utalii na ukarimu nchini kuzichangamkia na
kuzitumia teknolojia za kisasa kujikwamua na mathira ya janga la
Uviko-19 na kuiimarisha upya sekta hiyo muhimu ya utalii.
Maafisa
waandamizi wa Pesapal walitoa rai hiyo jana huku Zanzibar kwenye
mkutano shirikishi wa kwanza na wadau wa setka mzima ya utalii na
ukarimu.
Mkutano huo
ulihudhuriwa pia na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ambao waliipongeza
kampuni hiyo kwa kuchagiza matumizi ya huduma za kidijitali kwenye
utalii na kusisitiza umuhimu wa usalama wa mifumo ya malipo.
Katika
hotuba yake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Bw Omar Said
Shaaban, alisema ubunifu wa kiteknolojia na uwekezaji unaofanywa na
Pesapal unaendana na ajenda ya kidijitali ya serikali.
Kiongozi
huyo alibainisha kuwa wanaunga mkono kinachofanywa na kampuni hiyo
kwenye shughuli za ukarimu kwani jitihada hizo zinaunga mkono mikakati
na maono ya serikali ya kujenga uchumi wa kisasa ambao utategemea sana
mafanikio ya sekta ya utalii.
"Teknolojia
na shughuli za utalii na ukarimu ni pande mbili za sarafu moja. Wadau
wa utalii wanapaswa kukumbatia teknolojia za kidijitali ili waweze
kukabiliana na ubunifu unaofanyika katika sekta hii na kuweza kuyamudu
mahitaji mapya ya soko, ambayo yanabadilika kwa kasi sana,” Waziri
Shaaban alisisitiza.
Naye
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Bw Ali Suleimani Ameir, aliwasihi
wawekezaji wa teknolojia za kisasa kuhakikisha huduma zao zinasaidia
kukuza mapato ya serikali badala ya kuwa vyanzo kwa kupotea kwake.
Bw
Ameir alisema serikali za muungano na Zanzibar zimeruhusu matumizi ya
mifumo ya kidijitali kwa lengo la kurahisisha shughuli mbalimbali za
kiuchumi zikiwemo zile za kifedha hususani malipo na miamala mingine.
Aidha,
aliwataka washiriki wa mkutano huo wa Pesapal kuangalia njia na
uwezekano wa kupanua huduma za malipo ya kidijitali na kuimarisha
matumizi yake huko Zanzibar na Tanzania nzima kwa ujumla.
Mkutano
wa jana ulihusu zaidi kuangalia njia ambazo teknolojia mpya zinaweza
kusaidia kuimarisha uendeshaji na kuwa na vyanzo vipya na mbadala vya
mapato.
Wataalamu wa
Pesapal walitumia fursa hiyo kuwaonyesha na kuwahimiza wadau wa utalii
umuhimu wa teknolojia katika mipango yao ya kukuza biashara na mikakati
ya kuondokana na mathira ya Uviko.
Meneja
wa Pesapal Tanzania, Bi Bupe Mwakalunda, alisema kampuni hiyo ina
ushirikiano wa kimkakati na mashirika ya kimataifa kusaidia kutoa
suluhisho bunifu za kuimarisha huduma za utalii na ukarimu mara baada ya
kupungua sana kwa janga hilo lililoikumba dunia nzima.
“Uundaji
wa mifumo ya teknolojia inayoruhusu ubunifu wa haraka, kukuza faida na
kuongeza ufanisi itakuwa ni kipaumbele muhimu cha kujikwamua kutoka
kwenye janga ja Uviko-19 na kufikia ustahimilivu wa kidijitali,” Bi
Mwakalenda alibainisha.
“Ili
kufanikisha jambo hili, tumeshirikiana na Oracle Hospitality ili kutoa
suluhisho za kiteknolojia na kusaidia ushirikishwaji wa miundombinu
inayoweza kunyumbulika kutoa huduma thabiti na maalumu kwa ajili ya
wadau wa kisekta,” aliongeza.
Kongamano
hilo la kwanza la “Adopt & Thrive” liliwajumuisha washiriki
mbalimbali kutoka katika biashara za hoteli, migahawa, kumbi za starehe
na waongoza watalii.
Pesapal
na Oracle ni washirika wa karibu wa kuihudumia tasnia ya kusafiri na
ukarimu nchini kupitia utaalamu na suluhisho za teknolojia mahiri ili
kurahisisha na kuboresha huduma kwa watalii na wateja wengine kwa
ujumla.
No comments:
Post a Comment