Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema mfumo wa kielektroniki wa eGA tangu kuanzishwa umesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti upotevu wa mapato.
Mhandisi Ndomba, ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo ambapo amesema tangu kuanzishwa kwa mfumo huo umesaidia kudhibiti mianya ya ukwepaji wa malipo mbalimbali ya Serikali.
"Mfumo wa ukusanyaji wa Malipo ya Serikali Kielektroniki (GePG) ambao umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, mfumo huu unaimarisha uwazi na udhibiti katika ukusanyaji mapato ya Serikali,”amesema Ndomba
Aidha Mhandisi Ndomba amebainisha maeneo sita ya kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo amesema kama mamlaka itaendelea kusimamia sheria kanuni viwango na miongozo ya Serikali.
Aidha amesema Mamlaka itaandaa uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa umma.
MAMLAKA ya Serikali Mtandao ni Taasisi ya Umma ya utoaji wa huduma kwa wananchi yenye Lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Taasisi za Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa Umma ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuuk upitia TEHAMA.
No comments:
Post a Comment