HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 14, 2023

STEP waombwa kuharakisha ujenzi ukuta wa umeme Shoroba ya Tembo Kilombero


Waandishi wa hifadhi wa wanyamapori na utalii kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wakimsikiliza wanakijiji cha Sonjo Kata ya Mkula mkoani Morogoro, Mrashi Dongwe (aliyevaa mtandio mweupe).


Mfatiliaji wa taarifa za tembo Kijiji cha Kanyenja kitongoji cha Milesa mkoani Morogoro,  Juma Maumi, akionyesha kamera zilizofungwa karibu na hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa lengo la kuangalia njia za tembo.



Na Janeth Jovin, Aliyekuwa Mang'ula Morogoro 


SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) limeombwa kuharakisha ujenzi wa ukuta wa umeme katika Shoroba ya Tembo Kilombero inayounganisha hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere.


Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na wananchi wa Kijiji cha Sonjo, Sole, Mang’ula A na Kanyenja vilivyopo mkoani Morogoro mbele ya waandishi wa hifadhi wa wanyamapori na utalii kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) waliofanya ziara ya siku nne katika Shoroba ya hiyo.


STEP wamekuwa wakiwalipa watu fidia ili kupisha maeneo yao ambayo yapo karibu na shoroba hiyo ili kujenga ukuta huo wa umeme ambao utawazuia wanyama wakiwemo tembo kuingia katika mashamba ya vijiji kuharibu mazao na kudhuru watu.


Akizungumza na waandishi hao Mkazi wa Kijiji cha Sonjo Kata ya Mkula mkoani Morogoro, Mrashi Dongwe alisema wamekubali kutoa maeneo yao ili kupisha ujenzi wa ukuta wa umeme katika shoroba hiyo lakini wanaliomba shirika hilo kuharakisha mradi huo, ili kuwazuia tembo kuingia mashambani.


Alisema tembo wamekuwa ni kero kwani wanaingia katika vijiji na kuharibu mazao ambayo wanayategemea kuyavuna na kuuza ili kupata kipato kwa ajili ya kuendeshea maisha yao ya kila siku.


“Mimi sasa hivi kilimo ninakuwa nafanya kwa bahati nasibu, sina uhakika kama nitavuna kwani unaweza kulima ukitaka kukaribia kuvuna tembo wanakuja na kula karibu ekari nzima, tunawaomba hawa STEP waharakishe huu mradi wao kwani ukikamilika utatusaidia kuondoka na changamoto hii,” alisema Dongwe


Naye Mwajuma Issa mkazi wa kijiji cha Kanyenja alisema tembo wanasumbua hasa msimu wa mavuno ya mpunga hivyo wanaiomba Serikali kupitia STEP kuukamilisha kwa wakati mradi huo wa ujenzi wa ukuta wa umeme katika shoroba hiyo ili kuzuia matukio hayo.


“Tembo wakija wanaweza kula hata heka tano za mpunga kwa dakika, sasa hivi kila tunachokipanda ni shida wanakuja wanakula, hata hivyo tunawashukuru STEP wamekuja muda muafaka na mradi wao huu ambao kama utatekelezwa kwa wakati unakwenda kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hili,” alisema


Mohamed Libongoi mkazi wa kijiji cha Kanyenja kitongoji cha Mikoroshini alisema "Mwaka 1994 nimefika katika kijiji hiki kulikuwa hakuna tembo wanaokuja ila kuanzia 2011 hadi 2021 tembo wamekuwa huru sana kuja katika makazi ya watu, uwepo wa shoroba hii ya Kilombero utasaidia saba kuwadhibiti wanyama hawa,"


Mtendaji wa kijiji cha Mang'ula A, Yasinta Mlembe alisema katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kwenye kijiji hicho yametokea matukio mawili ya tembo kuharibu mazao mashambani. 


Alisema kuwepo kwa mradi huo wa ujenzi wa ukuta katika shoroba wao wanaona ni fursa pekee ya kumaliza changamoto hiyo ya tembo kuharibu mazao na kusababisha hasara kwa wakulima.


"Kupitia mradi wa shoroba wa wenzetu STEP utaweza kutusaidia kupunguza athari ya mnyama tembo kudhurura nakuharibu mazao yetu, kata hii ya Mangula ina vijiji viwili ila kijiji kinachoathirika zaidi na tembo Kanyenja kitongoji cha Milesa kwa sababu kipo karibu na hifadhi ya Taifa ya Nyerere," alisema


Kwa upande wake Meneja wa Shoroba ya Tembo Kilombero kutoka STEP, Joseph Mwalugelo alisema watahakikisha mradi huo wa ujenzi wa ukuta wa umeme unatekelezwa kwa wakati ili kumaliza changamoto hiyo inayowakabili wananchi hao.

Alisema wamekuwa wakifanya miradi mbalimbali ya kuhakikisha wanapunguza migogoro kati ya wanyama hasa tembo na wananchi wanaozunguka hifadhi hizo mbili.

“Tumekuwa tukifanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya jamii ambazo zinapakana na hifadhi, pia tunataka kupunguza kasi ya tembo kuingia mashambani na kuharibu mazao hivyo tumekuja na mradi huu wa ukuta wa umeme katika shoroba hii, tunaamini tutamaliza tatizo,” alisema Mwalugelo     

Ziara ya siku nne ya kutembelea  Shoroba hiyo imefanywa na waandishi hao kupitia mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tuhifadhi Maliasili chini ya usimamizi wa JET.

No comments:

Post a Comment

Pages