HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 22, 2023

TMA: Tunatarajia mvua zisizoridhisha masika

Na Irene Mark

KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a ametangaza uwepo wa mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi wakati wa masika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 22,2023 wakati akitoa taarifa ya utabiri wa msimu wa masika utakaoanza Machi hadi Mei mwaka huu, Dk. Chang’a alisema mvua hizo ni maalum kwa mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Dk. Chang’a alisema msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba.

Maeneo mengine ya nchi yanayopata mvua za masika ni ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.  

“Pamoja na utabiri huu kuonesha uwepo wa mvua zisizoridhisha wakati wa masika, baadhi ya maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha Mafia), kaskazini mwa Morogoro na kisiwa cha Unguja tinatarajia kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

“Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki na pili na ya tatu ya Machi na kumalizika wiki ya nne ya Mei mwaka huu... kwa baadhi ya maeneo mvua hizi zitaenda mpaka wiki ya kwanza ya Juni,” alisema Dk. Chang’a.

Kwa mujibu wa utabiri huo, ongezeko la mvua linatarajiwa zaidi Mei 2023, hasa maeneo ya pwani ya kaskazini mwa nchi.

Dk. Chang’a alizishauri mamlaka za kilimo na usalama wa chakula kuendelea kama ilivyo kawaida.

“Hata hivyo, kwa baadhi ya maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache zenye mtawanyiko hafifu, yanaweza kukumbwa na upungufu wa unyevu wa udongo na upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo na kuathiri uzalishaji wa mazao hasa katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Victoria.

“...Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi, kama mahindi na mazao jamii ya mikunde, hususani kwa mikoa ya pwani ya kaskazini inayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
 
“Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa masika,” alisema Dk. Chang’a.

Kupitia wadau TMA inashauriwa wakulima kuimarisha miundombinu ya kilimo na uvunaji maji ya mvua na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
 
Hata hivyo kila sekta imetakiwa kuzingatia taarifa ya utabiri huu na kuchukua hatua za tahadhari ili kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza kwa jamii na mazingira.


No comments:

Post a Comment

Pages