HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 08, 2023

WACHEZAJI WAPONGEZA KAMBI TIMU YA TAIFA MBIO ZA NYIKA


Mwenyekiti Kamisheni ya Wanariadha, Benjamin Michael (wa tatu kushoto), akiwa na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mbio za Nyika alipoitembelea kambini Mvono Lodge Ngaramtoni jijini Arusha. Kushoto ni Kocha Denis Male.



NA TULLO CHAMBO, RT


MWENYEKITI wa Kamisheni ya Wachezaji Shirikisho la Tanzania (RT), Benjamin Michael, ametembelea kambi ya Timu ya Taifa inayojiandaa na Mashindano ya Dunia, na kueleza kuridhishwa nayo huku akitoa pongezi kwa uongozi kufanikisha hilo.

Mashindano ya Nyika ya Dunia yanatarajiwa kufanyika nchini Australia Februari 18 mwaka huu, na kuelekea mashindano hayo, kikosi cha Tanzania kikiundwa na wanariadha wanne na kocha mmoja, kiliingia kambini rasmi Februari Mosi kwenye hoteli ya Mvono, Ngaramtoni jijini Arusha.

Wachezaji wanaounda timu hiyo ni Mathayo Sombi, Fabian Nelson, Inyasi Sulle na Josephat Gisemo huku Kocha ni Denis Male.

Akizungumzia kambi hiyo, Mwenyekiti wa Kamisheni, Benjamin Michael, amesema amekuta mazingira yanaridhisha na hali ya wachezaji iko vizuri.

"Nikiwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Wachezaji, leo Februari 8 mchana niliamua kutembelea kambi yetu ya mbio za Nyika iliyopo hapa Arusha....
Bahati nzuri nilifika nikakuta ndo wametoka mazoezi na wanapumzika kabla ya chakula cha mchana, nimeshiriki nao chakula kizuri, maji ya kutosha kila mchezaji ana katoni ya maji chumbani," alisema Michael na kuongeza.

Mazingira ya kambi ni mazuri, tulivu, yana huduma zote muhimu, karibu na maeneo ya mazoezi, kiukweli na nilivyowaona wachezaji wameridhika na ninategemea watakwenda kupambana vizuri.

Aidha, mbali na kuipongeza RT kwa kufanikisha kambi hiyo, aliwaomba jambo hilo liwe endelevu kwa timu nyingine za Taifa zitakazokuwa zinakabiliwa na majukumu mbalimbali ya kuliwakilisha Taifa kimataifa.

"Pamoja na kwamba hali inabana, niwapongeze RT kujikamua na kuiweka kambini timu hii, na hili liwe endelevu hata kama ni muda mchache, kuliko kuwaacha wachezaji wakiwa wanajiandaa kutokea majumbani," alisema Michael na kuongeza.

Pia naomba viongozi na wadau mbalimbali, siku zijazo uwekezaji uongezwe na kuimarishwa zaidi, ikiwamo timu ikiwa kambini iwe na mavazi rasmi, madaktari na huduma nyinginezo na anaamini hayo yanawezekana.

Timu hiyo, inatarajiwa kwenda jijini Dar es Salaam Februari 12, kabla ya kuagwa rasmi kisha kukwea pipa Februari 13 kwenda nchini Australia.

No comments:

Post a Comment

Pages