HABARI MSETO (HEADER)


March 23, 2023

MSOMERA KUWA KIJIJI CHA MFANO- WAZIRI MABULA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi mmoja wa wananchi wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga hati milki ya ardhi tarehe 22 Machi 2023.


Na Munir Shemweta, WANMM HANDENI

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga kitakuwa kijiji cha mfano kwa vijiji vingine nchini kwenda kujifunza kutokana na kuwekewa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kusimamiwa vizuri. 

 

Dkt Mabula alisema hayo tarehe 22 Machi 2023 wakati wa zoezi la kukabidhi  hati miliki za ardhi kwa wananchi waliohamia kijiji hicho kutoka Ngorongoro mkoani Arusha pamoja na wenyeji ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.

 

"Kijiji hiki sisi kama serikali chini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tunakwenda kukifanya kama kijiji cha mfano maana yake watu watatoka maeneo mengine kuja kujifunza hapa kutokana na namna kilivyopangwa na mnavyoisimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi" alisema Dkt Mabula.

 

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendekeo ya Makazi, wananchi waliopelekwa katika kijiji hicho cha Msomera kutoka Ngorongoro hawakupelekwa kwa bahati mbaya bali ni dhamira na nia njema ya serikali kumuwezesha mtanzania mmoja mmoja.

 

"Wote tunajua kabisa nia ya serikali ni njema, kitendo cha kuletwa na kuwa na uhakika wa ardhi kwa ajili ya kujenga na kupewa ardhi kwa ajili ya kilimo kwa ekari tano kwa kila kaya ni jambo la kumshukuru Mungu na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan. Alisema Waziri Mabula

 

Aidha, Dkt Mabula amewataka wananchi wa kijiji hicho kuepuka migogoro kwa kuwa Msomera ni eneo ambalo serikali inalitupia macho na kujifunza ambapo alisisitiza kuwa wizara yake haitaki kuona panakuwa na vijiji vinavyokuwa bila mpangilio.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya  Matumizi ya Ardhi Profesa Wakuru Magigi alisema,  awamu ya kwanza ya utekekezaji mradi kwenye kijiji cha Msomera, serikali imejenga takriban nyumba 503 na  viwanja vilivyopatikana eneo hilo  yaani kupangwa na kupimwa ni 4,620 huku viwanja  14,570 vikiwa vimebuniwa.

 

Kwa mujibu wa Profesa Magigi, katika viwanja hivyo kuna maeneo ya huduma mbalimbali ambapo alifafanua kuwa, viwanja vya makazi kila kimoja kina ukubwa wa ekari 2.5 lakini wakati huo huo kukiwa na maeneo ya mashamba yenye ukubwa wa ekari 5 ambapo maeneo hayo yanagawiwa kwa wananchi wanaohamia na wenyeji wa Msomera.

 

Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando alisema alipoingia wilayani humo alikuta migogoro kadhaa katika eneo hilo la kijiji cha Msomera hususan ile ya wenyeji na wageni ambapo ofisi yake ilichukua hatua ikiwemo kupitia nyaraka mbalimbali na kutatua changamoto hizo ambapo sasa wananchi wote wanaishi vizuri.

No comments:

Post a Comment

Pages