HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 03, 2023

WANANCHI HANANG’ WAMLILIA CHONGOLO AWASAIDIA NI BAADA KUCHUKULIWA MASHAMBA YAO KIUJANJA


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ambaye anaombwa na wananchi wa   wa vijiji vya Gaghata,Nyabat na Bassodesh Kata ya Bassodesh, wilayani Hanang' mkoa wa Manyara    kuingilia kati wapate sehemu ya maeneo ya mashamba ndani  ekari 1500 alizopewa mwekezaji ambaye ameshindwa kuziendeleza na wao kukosa maeneo ya kufanyia kilimo na ufugaji.

 

Dotto Mwaibale na Thobias Mwanakatwe, Hanang

WANANCHI wa vijiji vya Gaghata,Nyabat na Bassodesh kata ya Bassodesh, wilayani Hanang' mkoani  Manyara wamemliilia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo  wakimuomba aingilie kati kutokana  na kuchukuiwa mashamba yao mashamba yao zaidi ya ekari 1000 ambayo amepewa mwekezaji ambaye ameshindwa kuyaendeleza na kusababisha wakose maeneo ya kulima na kufugia mifugo yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti ambao walifika katika vijiji hivyo, walisema maeneo hayo alipewa mwekezaji wa  ambaye ni Hospitali ya Hydom (Hydom Lutheran Hospital) inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) na viongozi wa kijiji hicho tangu mwaka 1992 lakini hayaendelezwi na badala yake wamekuwa wakiyakodisha.

Walisema wamelazimika kumuomba Chongolo aingilie kati mgogoro huo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 30 bila kupatiwa ufumbuzi ambapo viongozi wa wilaya hiyo mwishoni mwa mwezi wa Februari, 2023 walilazimika kwenda katika kijiji cha Basidosh kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho baada ya vyombo vya habari kuibua sakata hilo hilo baada ya mkazi mmoja wa eneo hilo, Qwari Sulle kulalamika ngazi ya juu kufuatia eneo lake alililoachiwa na baba yake aliyekuwa akilimiliki tangu mwaka 1979 kabla ya mwekezaji huyo kufika mwaka 1992..

Walisema katika hali ya kushangaza kila wanapokwenda kulalamikia haki yao katika ngazi nyingine za serikali baadhi ya viongozi wakiwamo wanasiasa wastaafu ambao wanatajwa kuhusika katika mgogoro huo baada ya kumpa mwekezaji huyo wamekuwa wakitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao huenda kuwakamata na kuwaweka ndani hasa mwananchi ambaye ameonekana kuwa mstari wa mbele kufuatilia suala hilo na tayari mapema mwezi huu amepelekwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya jinai.

Mapema mwezi uliopita mwananchi  Qwari Sulle alipata kadhia ya kukamatwa na polisi wa kituo cha Bassotu na baadaye kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Hanang' ambako alilala huko hadi siku ya pili alipoachiwa kwa kujidhamini mwenyewe na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Katabazi kuthibitisha tukio hilo.

Sulle ambaye eneo lake la ardhi la ekari 32 ambazo anadai zimechuliwa na mwekezaji huyo inaelezwa aliwekwa ndani kituo cha polisi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni agizo kutoka kwa kigogo mmoja wa serikali wilayani kufuatilia kiongozi mmoja wa kisiasa mstaafu  kulalamika kuwa mwananchi huyo aliwapeleka wanahabari kijijini hapo.

Sulle alisema mwishoni mwa Desemba mwaka jana alikwenda kupeleka malamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya Hanang’, Janeth Mayanja ambaye alimtaka aandike barua ya malamiko ambayo aliiandika na kumkabidhi Katibu Tawala wa wilaya hiyo John Bura kama alivyoagizwa na mkuu wa wilaya lakini kila alipokuwa akienda kuulizia hakupewa majibu yoyote ndipo alipoamua kwenda ngazi nyingine na kwa vyombo vya habari kulalamika jambo lililouibua uongozi wa wilaya hiyo na kufika kijijini hapo.

Mbali ya Sulle kulalamikia jambo hilo linalohusu eneo lake la ekari 32 zilizochukuliwa na mwekezaji huyo wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakifuatilia jambo hilo tangu mwaka 1990 ambapo Oktoba 15, 2012 waliandika barua katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Hanang' kuomba wasaidiwe suala hilo lakini hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana.

"Mwekezaji huyu wakati anapewa mashamba hayo mwaka 1992 yaliwekwa makubaliano kati ya serikali ya vijiji hivyo ambavyo awali kilikuwa ni kijiji kimoja cha Basodesh kuwa awajengee lambo la kunyweshea mifugo, wajengewe zahanati na shule lakini hadi leo hii ni miaka 30 imepita hajatekeleza makubaliano na wala kuyaendeleza mashamba hayo ambayo sehemu kubwa ni msitu na hata hayo yanayolimwa ni yale yanayokodishwa kwa wananchi na hospitali hiyo" alisema mmoja wa wananchi hao.

Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata ya Basodesh, Patrick Amo akizungumza katika mkutano huo wa utatuzi wa mgogoro huo uliotwishwa na mkuu wa wilaya hiyo alisema hospitali hiyo imepoteza sifa ya kumiliki mashamba hayo kutokana na kushindwa kutekeleza makubaliano na kuyaendeleza mashamba hayo kwa zaidi ya miaka 30.

Amo aliongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa watu na ardhi kuwa ndogo na mwekezaji huyo kuwa na ardhi kubwa ambayo haiendelezi alimuomba mkuu wa wilaya hiyo kuangalia namna bora ya kutatua mgogoro huo.

Aidha, Amo alimuomba mkuu wa wilaya kuangalia namna ya kumsaidia eneo mzee Sulle Tlehhema ambaye aliahidiwa na serikali ya kijiji kuwa angepewa eneo lingine baada ya lile alilokuwa akilitumia kwa malisho ya mifugo YAKE na kilimo kupewa mwekezaji.

Alisema hivi sasa kijiji hicho hakina ardhi hivyo kama itafaa hospitali hiyo ikate sehemu na kumuachia mzee huyo ekari hizo 32 alizompa mtoto wake Qwari ambazo zipo mpakani mwa shamba hilo na kijiji kingine.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Taghata Nestory John alisema mgogoro huo ambao umedumu kwa muda mrefu umesababisha wananchi kukataa misaada inayotolewa na hospitali hiyo kama kujenga ofisi ya kijiji wakidai ni danganya toto kwa kuwa imechukua ardhi kubwa na kuwaacha wananchi wakiwa hawana mashamba wala maeneo ya kilimo.

Katibu wa CCM Kata ya Basodesh, Paul Silaa alisema mgogoro huo sio mkubwa kwa kiasi hicho ambapo alimuomba mkuu wa wilaya hiyo kuona namna ya kumsaidia mzee Tlehhema kupata eneo aliloahidiwa na serikali ya kijiji hicho wa wakati huo pamoja na mama Katelina Salimee ambaye naye alikuwa na ekari 20 ambazo zimechukuliwa na hospitali hiyo.

Mzee Sulle Tlehhema baba mzazi wa Qwari mwenye umri wa miaka 110 akizungumza kwenye mkutano huo alisema alifika kwenye eneo hilo mwaka 1979 na kulikuwa na watu wa kuhesabu na mwaka 1992 ndipo alipofika mwekezaji huyo na hata walipokuwa wakichonga barabara za kuweka mipaka alikuwepo katika eneo hilo.

Mzee Tlehhma alisema wakati walipokuwa wakiweka mipaka hiyo alipowauliza viongozi wa kijiji wa wakati huo akiwepo katibu kata mzee Elisha walimuambia watamtafutia eneo lingine mbadala na hilo na kuwa hadi leo hii kijiji hicho hakijampatia eneo lolote na hajui hatima yake ni  nini na anaumia sana anapoona mtoto wake akipata misukosuko ya kukamatwa bila ya kujua aende akaishi wapi na familia yake pamoja na mifugo.

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Hanang', Janeth Mayanja , ambaye aliambatana na baadhi ya wataalamu kutoka katika ofisi yake na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama akitangulia kuvilaumu vyombo vya habari kwa kutoa taarifa ya mgogo huo alisema mashamba hayo mmiliki halali ni hospitali hiyo.

"Kwa mujibu wa vielelezo nilivyonavyo mmiliki wa mashamba hayo ni Hospitali ya Hydom na wameyapata kwa kufuata taratibu zote na kuna muhutasari wa makubaliano kati ya serikali ya kijiji wakati huo na wanahati ya kumiliki mashamba hayo iliyotolewa na wizara ya ardhi miaka 2000" alisema Mayanja.

Mayanja alisema anaipongeza hospitali hiyo kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwapatia wananchi mashamba hayo kwa ajili ya kuyalima kwa kufuata utaratibu wa kuandika majina yao.

Hata hivyo, alimshukia mwekezaji kwamba kitendo cha kuwakodisha mashamba wananchi kinazidisha vurugu.

Aidha Mayanja aliomba mwekezaji huyo aongezewe muda zaidi wa kutekeleza makubaliano aliyotakiwa kuyatekeleza tangu mwaka 1992 ya kujenga lambo, zahanati na shule na aliwaomba wafanya haraka nawananchi waendelee kuwa na imani na mwekezaji huyo na kuanza kupokea misaada yake ikiwemo ya miradi ya maendeleokama kuchimbiwa visima vya maji na kujengewa ofisi ya kijiji na kwa kutofanya hivyo ni kujicheleweshea maendeleo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja akizungumza na wananchi wa Kata ya Basodesh wakati wa utatuzi wa mgororo huo wa ardhi dhidi ya vijiji hivyo.
Muonekano wa baadhi ya mashamba ambayo yamelimwa na wananchi kwa njia ya kukodishwa na mwekezaji.


 Ni moja ya shamba ambalo lilikuwa lake ambalo amelima mahindi ili kujikimu na njaa lakini limesababisha kukamatwa na polisi akidaiwa kulilima kinyume na utaratibu na kufunguliwa kesi ya jinai.


Qwari Sulle (kulia) ambaye amekuwa akipata adha ya kukamatwa mara kwa mara na polisi wakati akifuatilia haki ya kupata shamba lake na kufunguliwa kesiya jinai akiwa na familia yake na mama yake mzazi nje ya nyumba yake. Qwari hana hata sehemu ya kulima baada ya mashamba yake yote kuchukuliwa na kubakiwa na nyumba zake na hajui hatima ya maisha yake.

 

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Hanang' wakibadilishana mawazo wakati wa utatuzi wa mgogoro huo katika Kata ya Basodesh.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo wakiwa Kijiji cha Basodesh kutatua mgogoro huo uliodumu kwa miaka 30.
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata ya Basodesh, Patrick Amo akizungumza katika mkutano huo.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Mzee Elisha Wee ambaye alikuwa kiongozi wa kijiji hicho ambao walimpa mwekezaji shamba ekari 1500 akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkazi wa kijiji hicho Emmanuel Sulle akizungumza mashamba hayo ambayo wanayamiliki tangu mwaka 1979.
Mzee Tlehhema Sulle baba mzazi wa Qwari aliyempatia mwanaye huyo shamba la ekari zaidi ya 90 ambalo alianza kuliendeleza tangu mwaka 1979 kabla na baadaye kuchukuliwa na hospitali hiyo ya Hydom inayomilikiwa na KKKT wakidai ni lao baada ya kufika katika kijiji hicho mwaka 1979
Mwenyekiti wa Kijiji cha Taghata Nestory John akizungumza kwenye mkutano huo.
, Mbunge wa Hanang' Mhandisi Samweli Xaday (kulia) akiteta jambo na Mzee Sulle Tlhhame ambaye aliahidiwa kupewa mashamba mbadala na kijiji hicho lakini hadi leo hii hajapewa na anatakiwa kuondoka katika eneo lake alilokuwepo tangu mwaka 1979., 

No comments:

Post a Comment

Pages