Waziri wa afya Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera juu ya mikakati ya Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Marburg.
Na Alodia Babara, Bukoba
Wananchi waliowekwa karantini wanaofuatiliwa viashiria vya Marburg wameongezeka kutoka 193 hadi 205 huku Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisema hakuna wagonjwa walioongezeka.
Waziri Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya mkuu wa mkoa leo Machi 25, 2023 amesema kuwa, wataalamu wa afya wanaendelea kufuatilia watu wote waliochangamana na wagonjwa wa Marburg na kuwaweka karantini kwa kipindi cha siku 21 ili kubaini kama wana dalili za ugonjwa huo ambao mtu anaambukiza baada ya kuonyesha dalili.
Amesema, kutokana na kiini cha mgonjwa kutokea kisiwa cha Gozba tumetuma timu ya wataalamu kutoka wilaya ya Muleba ambao watafanya ufuatiliaji kubaini wale wote waliochangamana na mgonjwa huyo ambaye baada ya kutoka kisiwani alienda kwenye familia yake Maruku.
Amesema wametuma madatari bingwa wabobezi sita hapa Kagera miongoni mwao wamo dk bingwa wa magonjwa ya ndani na dk bingwa wa moyo.
Mwalimu aliwataka wakazi wa mkoa wa Kagera kuendelea na shughuli zao za kila siku na kutokuwa na hofu na ugonjwa huo na akawataka kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono na kutogusana mikono ni pamoja na kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa afya.
Amesema Wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 1322 wamepata ajira ya muda wa miezi mitatu mkoani Kagera kwa ajili ya kusaidia Kutoa elimu ngazi ya jamii katika kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Marburg.
‘Katika juhudi za serikali za kupambana na ugonjwa wa Marburg tutayatumia makundi matatu ambayo ni wahudumu wa afya ngazi ya jamii, viongozi wa dini na waganga wa kienyeji na tumeajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 1322 ambao watakuwa katika mkoa mzima lakini kwa sasa tumeanza na halmashauri mbili Bukoba vijijini na Bukoba manispaa na wahudumu hao tutawaweka kila kitongoji wawili, mtaa watatu na kila kijiji mmoja” Amesema waziri Mwalimu
Aidha kwa upande wa mganga mkuu wa mkoa dk Issesanda Kaniki amesema kuwa, kwa kushirikiana na manispaa ya Bukoba pamoja na wadau wengine watafanya mwendelezo wa kuweka vifaa vya kunawia mikono katika maeneo ya kituo kikuu cha mabasi pamoja na soko kuu na katika barabara ya magari yaendayo Geita, Mwanza Kahama, Dar es salaam na mikoa mingine kitawekwa kituo maeneo ya kemondo ili abiria wote wapimwe joto na barabara ya kwenda Karagwe, Mtukula pia eneo la Kyaka Misenyi kitawekwa kituo cha kupima abiria wote wanaotokea barabara hiyo.
Waziri Mwalimu atatembelea kata ya Maruku na Kayangereko ambapo walipatikana wagonjwa wa Marburg na atatembelea eneo ambalo watu 205 wamewekwa karantini pamoja na kituo cha matibabu ya wagonjwa wa Marburg.
Ikumbukwe kuwa Machi 15 watu nane walibainika kuugua ugonjwa usiojulikana na watu watano walipoteza maisha na Machi 21 mwaka huu serikali ilitangaza rasmi kuwepo ugonjwa wa Marburg ambapo hadi sasa serikali kupitia wataalamu wa afya wameendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na wagonjwa watatu wanaendelea na matibabu.
No comments:
Post a Comment