HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 10, 2023

JOWUTA, LHRC kufungua kesi kuwatetea wafanyakazi Sahara Media

>Serikali pia kuwafikisha mahakamani kwa deni la 2.5 bilioni

Ofisa kazi kiongozi mkoa Mwanza Betty Mtega akipeana mkono na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma alipomtembelea ofisini kwake.
 

Mwandishi Wetu, Mwanza

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimetangaza kushirikiana na Kituo Cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) kuwasaidia wafanyakazi 195 wa Kampuni ya Sahara Media kudai  malimbikizo ya mishahara yao kiasi cha sh 3.5 bilioni.

Uamuzi huo, umetangazwa Jana na Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma na Mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa JOWUTA, Mutta Robert katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa Chama cha Ushirika  Nyanza, baada ya kukutana na pande zote katika mgogoro huo.

Juma amesema baada ya majadiliano baina ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na ofisi ya Idara ya kazi mkoa wa Mwanza na LHRC  wameazimia kupeleka mgogoro huo katika Tume ya Usuluhishi (CMA) 

"Kwa kuwa mwajiri hajakaidi kulipa deni hili na ameshindwa kulipa licha ya kuahidi kufanya hivyo hali yake ya fedha itakapokuwa nzuri, tumeona njia bora ni kupeleka shauri hili CMA"amesema 

Amesema JOWUTA kama chama cha wafanyakazi itashirikiana na LHRC na wanasheria wengine ambao tayari wameonesha nia Ili kuhakikisha haki za wafanyakazi hao zinapatikana .

Juma amesema wamefikia uamuzi ili kulinda heshma ya Tasnia ya Habari nchini, kwani kwa sasa ni miongoni mwa sekta ambazo zinachangamoto kubwa ya malipo na stahiki za waandishi na watangazaji kwani wengi hawana mikataba licha ya kufanya kazi miaka mingi.

"JOWUTA  tunaamini kesi hii ya Mwanza itakuwa ni mfano wa kesi nyingine ambazo zitafuata katika kulinda na kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini, kwani hadi sasa kuna waandishi wanaolipwa shilingi 1000 kwa habari moja na wengi hawalipwi kabisa na kubaki kutegemea kulipwa na wanaowapa habari,"amesema

Amesema Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari wanastahiki kupata heshma na hadhi sawa na wafanyakazi wa sekta nyingine kwani licha ya serikali kutunga sheria za kazi na sheria za vyombo vya habari lakini bado wanahabari wanataabika.

"Wanahabari licha ya kufanya kazi kubwa bado asilimia 80 hawana ajira za kudumu wala mikataba tofauti na taaluma nyingine hali ambayo imekuwa ikiathiri utendaji wao wa kazi"amesema

Amesema wakati wamiliki wa vyombo vya habari wakililia uhuru wa vyombo vya habari  na kulipwa malimbikizo ya madeni ya matangazo wanapaswa kutambua kuwa uhuru huo hautakamilika kama wanahabari wakiendelea kuwa na maslahi duni, kufanya kazi bila mikataba na kutolipwa mishahara.

"Tunataka katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu suala la maslahi bora kwa wanahabari lipewe kipaumbele  kwani uhuru wa vyombo vya  habari hauna maana kama hakuna maslahi bora kwa wanahabari, tunaiomba serikali kuchukuwa hatua kwa wamiliki ambao hawazingatii sheria licha ya kupata mapato katika vyombo vyao,"amesema.

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini JOWUTA, Mutta Robert alisema watatumia sheria za kazi kufungua mashauri katika vyombo vyote vya habari ambavyo havilipi wanahabari.

"Sheria za kazi zipo tutahakikisha tunazitumia kulinda heshma ya taaluma hii kwani kuna wamiliki wa vyombo vya habari wanawatumia wanahabari kama vitega uchumi vyao,"amesema

Robert ambaye pia ni Mwanasheria amesema sheria zipo wazi na lazima zifuatwe na wamiliki wa Vyombo vya Habari na kesi ya Mwanza itakuwa mfano kwa wamiliki wengine ambao hawazingatii sheria za kazi.

Wakili Hamisi Mayomba wa LHRC amesema tayari taratibu za kufungua shauri hilo zimeanza na ambacho kinasubiriwa kukamilishwa kwa nyaraka mbalimbali ambazo zitasaidia katika shauri hilo.

Awali Ofisa Kazi Kiongozi mkoa wa Mwanza, Betty Mtega alisema ofisi yake imechoshwa na mashauri ya wanahabari kushindwa kulipwa stahiki zao.

"Tumekuwa na kesi ya Sahara Media na vituo vingine vya radio  hawataki kufuata sheria kuwalipa wafanyakazi wao licha ya kukiri kudaiwa,"amesema

Hata hivyo amesema serikali haijakaa kimya na shauri la Sahara Media kwani hivi karibuni litafikishwa mahakamani na ofisi ya Mwanasheria Mkuu Kanda ya Ziwa.

"Kamishna wa kazi nchini tayari amekamilisha taratibu zote za shauri hili kufikishwa vyombo vya sheria na kumbukumbu zetu hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2021 wafanyakazi 152 walikuwa wanadai zaidi ya sh 2.5 bilioni na mwajiri amekiri kudaiwa,"amesema.

Hata hivyo amesema deni hilo limekuwa kubwa kutokana na wanahabari kutojua sheria za kazi kwani walipaswa kufungua mashauri mara tu wanaposhindwa kulipwa kwa miezi miwili.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuwaamini wafanyakazi wao kuhakikisha wanawaajiri na kuwapa mikataba bora.

"Mwanahabari bora ni yule ambaye pia uchumi wake upo vizuri hivyo wamiliki wakiwalipa vizuri wafanyakazi wao wataweza kufanya kazi kwa weledi mkubwa,"amesema

Hata hivyo Soko amewataka wanahabari nchini kujiunga na JOWUTA kwani kisheria ndio chama pekee cha wafanyakazi ambacho kinadhamana ya kutetea maslahi yao.


No comments:

Post a Comment

Pages