HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 20, 2023

DC YOHANA AWATAKA WANA HABARI KAGERA KUTOSHINIKIZWA KUTOA TAARIFA ZISIZO SAHIHI

Na Lydia Lugakila, Bukoba

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Yohana Siima, amewataka Wanahabari Mkoani humo, kutoshinikizwa na mtu yeyote, kutoa taarifa zisizo sahihi, zinazoweza kuhatarisha amani iliyopo hapa nchini.

Siima ametoa kauli hiyo, akiwa Mgeni rasmi, katika maadhimisho ya Uhuru wa Habari, kwa Chama Cha waandishi wa habari, Mkoa wa Kagera KAGERA PRESS CLUB, yaliyofanyika katika ukumbi wa Bukoba Coop, uliopo Manispaa ya Bukoba mkoani humo.

DC Siima, amesema kuwa, wakati Wana habari wakiadhimisha siku hiyo, wanatakiwa kutoshinikizwa na mtu yeyote, kwani madhara yake ni makubwa, ikiwemo kukosekana kwa amani,badala yake watoe taarifa sahihi na zenye ukweli  ambazo hazijahusisha upande mmoja, na zisizo potosha umma.

Ameongeza kuwa, Wanahabari ni lazima watimize majukumu yao kwa kuzingatia weledi, ambao wameupata kupitia taaluma yao, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa wakati, ili jamii inufaike na vyombo hivyo.

Aidha amewashuru wanachama wa Kagera Press Club, pamoja na waandishi wa habari wengineo, kwa namna walivyotoa ushirikiano  kwa Serikali, katika kutoa habari pamoja na kuwa mstari wa mbele, kufuatilia matukio mbali mbali yaliyoutangaza Mkoa huo, huku akiahidi kuwapa ushirikiano mkubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha waandishi wa habari Mkoa wa Kagera, Mbeki Mbeki amewasisitiza Wana habari hao, kuendelea kutimiza wajibu wao, kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali, wa Habari pamoja na serikali

Mbeki Ametumia nafasi hiyo kuwaomba waajiri wa vyombo vya habari Mkoani humo kuwajali na kuwathamini wafanyakazi wao pindi wanapatwa na matatizo wakiwa kazini.

 Naye Respicius John ambaye ni mwandishi wa Habari Mkoani humo, amewashauri Wana habari hao, kuwa mstari wa mbele, kufichua vitendo  vya ukatili vinavyoendelea katika Jamii.

Hata hivyo naye Mutayoba Albogast kwa niaba ya wana habari, ameahidi kuyafanyia kazi yote yaliyozungumzwa na Viongozi hao huku akisisitiza ushirikiano.

Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya Uhuru wa vyombo Habari Duniani, ambao kila mwaka hufanyika mei 3, kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika visiwani Zanzibar, huku yakibeba kauli mbiu isemayo, "Kuunda Mustakabali wa Haki " Uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha haki nyinginezo za kibinadamu.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Yohana Siima akizungunza katika maadhimisho ya Uhuru wa  vyombo vya Habari.

No comments:

Post a Comment

Pages