Makabidhiano ya Ofisi kati Albert John Chalamila Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Fatma Mwassa Mkuu mpya wa Mkoa wa Kagera.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert John Chalamila (kushoto) akiweka saini vitabu maalum vya mkoa huo ili kumkabidhi Ofisi Fatma Abubakar Mwassa Mkuu mpya wa Mkoa wa Kagera.
Na Lydia Lugakila, Bukoba
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert John Chalamila amefanya makabidhiano ya Ofisi kati ya Fatma Abubakar Mwassa ambaye ndiye Mkuu wa Mkoa huo huku akiahidi kufufua na kuendeleza vyema miradi ya maendeleo.
Hafla hiyo ya Makabidhiano hayo imefanyika katika ukumbi wa Mkoa huo ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Abubakar Mwassa kuendeleza mshikamano kwa Wananchi na watumishi wa Mkoa huo katika kuhakikisha miradi aliyoiacha inaendelezwa vyema na nyingine kufufuliwa kwa manufaa ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Rc Chalamila amesema kuwa anaondoka Kagera akiwa na utambuzi huku akiamini miradi mbali mbali ya maendeleo itaendelezwa ikiwemo ujenzi wa Soko, Stendi Chuo kikuu na ujenzi wa Bandari kuendelezwa ikiwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro ya Ranchi kati ya wakulima na Wafugaji sambamba na Kupambana na suala la udumavu.
"Nawashukuru sana Wananchi na watumishi wa Mkoa huu kwa ushirikiano mliouonyesha kwa miezi hii 9 niliyokaa na kuitumikia Kagera hakika nimevuna Baraka asante sana Rais Samia kwa imani hii kubwa kwangu ushauri wangu kwa Fatma Mwassa usiogope kutekeleza majukumu yako hapa Kagera" alisema Chalamila.
Ameongeza kuwa ili mji huo wa Bukoba ubadilike ni lazima pawepo mshikamano wa pamoja huku akiwasisitiza wakazi wa Mkoa huo waliopo Jijini Dar es Salaam kuitika na kurudi kuujenga Mkoa huo kiuchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Abubakar Mwassa amewaomba watumishi wa Mkoa huo kumpa ushirikiano huku akiwaondoa wasi wasi wananchi Mkoani humo kuwa wamuamini kwani atahakikisha Miradi yote inatekelezwa kwa wakati ikiwemo ujenzi wa Stendi, Soko, Chuo kikuu na kuendeleza upanuzi wa Bandari zote.
"Mimi sio Muumini wa kuongea Mimi huwa ni Muumini wa kutenda Sana, naamini wasaidizi wangu mliulizia nilikotoka nasema Hapa ni kazi kazi buti buti hakuna hadithi" alisema Fatma Mwassa.
Amechukua nafasi hiyo kuwaomba Wananchi Mkoani humo kulima mazao ya thamani kubwa ili yaongeze kipato ikiwa ni pamoja na kutumia fursa kubwa ya kuongeza nguvu kwenye uvuvi wa samaki na dagaa huku akiahidi kukuza na kulitangaza soko la Senene ndani na nje ya nchi.
"Tumezoea wengi waliokuja hapa kuuongoza Mkoa huu ni wanajeshi na ni wanaume, sasa Mimi Mwanamke na si mwanajeshi nimekuja kupiga kazi" alisema Fatma.
Naye Mzee Pius Ngeze akitoa neno kwa niaba ya Wazee wa Mkoa wa Kagera amempongeza Rc Chalamila kutokana na dhamira yake ya kuvipigania vyuo vikuu ili vifufuke, Kupambana na kero za beria, kusimamia vyema kuanzishwa kwa chuo kikuu huku akimuomba kuendeleza mema katika uongozi wake.
Hata hivyo Mzee Pius amemsihi Mkuu wa Mkoa huo Fatma Abubakar Mwassa kuendeleza mazuri ya Chalamila ikiwa ni pamoja na kuinua kipato cha Wananchi wakulima kinachoonekana kuwa chini pamoja na kuupambania vyema Mkoa huo ili kuondokana na umaskini.
No comments:
Post a Comment