HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2023

Ikolojia yaathiriwa na viumbe vamizi

Na Selemani Msuya


MENEJA wa Kitengo cha Sera za Usimamizi wa Maliasili mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Joseph Olila amesema ongezeko la viumbe vamizi kwenye hifadhi, mimea na wanyama vimesababisha mfumo ikolojia kubadilika, hivyo kuwa changamoto katika mazingira, uchumi na jamii.

Olila amesema hayo jijini Dar es Salaam Juni 21 2023, wakati akiwasilisha mada katika mjadala wa asubuhi kuhusu Uhifadhi wa Bioanuai kwa waandishi wa habari, iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).


Meneja huyo ambaye aliwasilisha mada inayohusu Changamoto ya Viumbe Vamizi katika Uhifadhi na Maendeleo ya Jamii, alisema juhudi zinahitajika kukabiliana na ongezeko hilo kwa kuwa madhara yake ni makubwa.


Amesema changamoto ya mazingira imesababisha kupungua kwa bioanuai ambapo matokeo yake ni mfumo ikolojia kubadilika na viumbe kukosa chakula katika mtiririko sahihi wa kimfumo.


“Viumbe vamizi wanachangia uharibifu wa makazi wa viumbe, hivyo uendelevu wa viumbe unapata changamoto, lakini pia huchangia usambazaji wa magonjwa kwa mimea na wanyamapori,” amesema
Olila amesema madhara ya viumbe vamizi kwenye jamii ambapo huchangia mambo mengi kama kupoteza tamaduni, ufugaji, magonjwa kwa binadamu au mzio, kupoteza mali kama mazao na mifugo.


“Changamoto ya kiuchumi inaonekana kwenye biashara na serikali kutumia fedha nyingi kudhibiti, kusimamia, kupunguza uzalishaji, hivyo kuongeza bei ya vyakula, kuathiri sekta ya utalii, kuongeza gharama za matibabu na nyingine nyingi,” amesema. 


Meneja huyo amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira iliandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Viumbe Vamizi wa miaka 10 ambao umeanza 2019 hadi 2029.


Olila amesema katika kufanikisha mpango mkakati wamekubaliana kuweka vipaumbele sita kwenye baadhi ya mimea kama Mathenge (Prosopis juliflora) kwa ajili ya sekta ya mifugo ambao uliingia Tanzania 1950 ili kuzuia mmomonyoko.


Amesema katika sekta ya misitu wameweka mkazo kwenye miti aina ya Lantana Camara, Gugu maji ambayo yalihusisha sekta ya maji na usafiri kuanzia mwaka 1960.


Naye Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa USAID Tuhifadhi Maliasili, John Noronha amesema mafunzo ambayo wanatoa kwa waandishi wa habari kuhusu uhifadhi na ushoroba yanalenga kuwajengea uwezo wa kuandika kwa umakini na usahihi habari kuhusu sekta hiyo.


Noronha amesema iwapo waandishi wa habari watafikisha habari sahihi kwa jamii kuhusu eneo hilo ni wazi taarifa za kupotosha kuhusu wanyamapori na wananchi zitapungua kama sio kuisha kabisa.
“Hii mada ya Uelewa kuhusu Migogoro ya Binadamu na Wanyamapori na Namna ya Kuitatua inatakiwa kufika kwa wananchi kwa ufasaha ili kujenga jamii yenye kwenda kwa pamoja,” amesema.


Aidha, Noronha amesema pia kuna umuhimu wa kusimamia sheria, kanuni na taratibu zote ambazo zinahusika katika sekta ya wanyamapori na uhifadhi kwa kuwa zimezingatia usawa na haki.
Naye Ofisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Dar es Salaam, Msafiri Kasara amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanahusisha kundi lenye mchango mkubwa katika kuelimisha jamii.


“Sisi tunaungana na wadau wote ambao wanapigania usalama wa wanyama na wananchi, kwani bila kushirikiana ni ngumu sana kupambana na ujangili na uvinjifu wa sheria,” amesema.
Amesema pia TAWA inahusika na kutangaza utalii kwa kufuata njia sahihi ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Wanyamapori ya 2007, Sera ya Utalii ya 1999, Sheria ya Wanyamapori ya 2009 na kanuni na mpango mkakati (2021/2022-2025/26).


Ofisa Mwandamizi wa TAWA, Weja Lugendo amesema majukumu mengine ya mamlaka hiyo kuhakikisha wanyamapori wanalindwa ili wasidhuriwe na majangili.


Amesema wanashirikiana na Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wengine kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu na wanyama wanakuwa salama,


Aidha, amesema wanasimamia utalii wa kuwinda na picha katika maeneo ya Serikali na wanavijiji kupitia (WMA) ambao umeonesha matokeo chanya.

No comments:

Post a Comment

Pages