HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 15, 2023

Mchango wa sekta binafsi katika Afya ni mkubwa: Waziri Ummy

 Na Mashaka Mhando, Tanga


WAZIRI wa Afya na mbunge wa jimbo la Tanga, Ummy Mwalimu amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itaweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi katika kutoa huduma za afya ili kuokoa maisha ya watanzania. 

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaimu, akifungua jengo la wagonjwa wa nje katika hospital binafsi ya Safi Medics iliyopo jijini Tanga. 


Waziri Ummy amesema kuwa mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya ni mkubwa hivyo serikali itahakikisha inaondoa vikwazo na kuwawekea mazingira wezeshi yatakayoweza kuwasaidia kutoa huduma bora za afya kwa watanzania walio wengi. 


"Niwapongeze sana Safi Medics hospital kwa kuwekeza hispitali hii ya kisasa katika Halmashauri yetu ya jiji la Tanga na sisi kama serikali tutaendelea kuwatambua ikiwemo serikali imetoa msamaha wa riba kodi kwa vifaa tiba vyote pamoja na dawa zinazoingizwa ndani ya nchi kwahiyo ni dhamira ya serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba watanzania wanapata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha, "alisisitiza Waziri Ummy Mwalimu. 


"Tuwashukuru sana Safi Medics Dkt Mberesero na timu yako hongereni sana na kama kuna jambo lolote na vikwazo mnapitia serikali ipo tayari na itawapa kipaumbele ili muendelee kuwatimikia Watanzania, "alisema Waziri Ummy. 


Aidha Waziri Ummy amewasisitiza watanzania kujiunga na mifuko ya bima za afya ili kuweza kuwa na uhakika wa matibabu bila kikwazo chochote kile cha fedha. 


Waziri Ummy amesema serikali ya awamu ya sita imeweka huduma ya siti skan katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo ambapo hapo awali wakazi wa Tanga walikuwa wakilazimika kwenda jijini Daresalaam au Mkoani Kilimanjaro kufuata huduma hiyo. 


"Chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tumefunga siti skani mashine katika Mikoa yote ya Tanzania bara lakini pia huduma za kusafisha damu watu walikuwa wanakwenda Daresalaam au Kilimanjaro lakini hivi sasa zinapatikana Bombo na nimeona Safi Medics nao wapo mbioni kuweka huduma hiyo, "alisema Waziri Ummy. 


Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika hospital binafsi ya Safi Medics hospital,  Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaimu, amesema kuwa mwenge wa uhuru umepokea taarifa ya kina ya inayohusiana na mradi huo ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi mradi husika ili kubaini ubora na viwango vya mradi wenyewe sambamba na kuangalia vifaa tiba ambavyo kimsingi vitatumika katika utoaji wa huduma ya afya. 


" Tumeangalia pia namna ya matumizi na thamani ya fedha ambayo imetumika katika mradi huu itoshe kwa dhati mheshimiwa Waziri na Mkuu wa Wilaya hii itoshe tu kusema kuwa niwashukuru  wenzetu wa wa Safi Medical hospital  kwa uwekezaji huu ambao kimsingi unao dhamira ya dhati ya kuokoa maisha ya watanzania, 


"Serikali pendwa imewawekea mazingira wezeshi na rafiki ili kuona wenzetu wa taasisi binafsi mnaendelea kushirikiana na serikali katika utoaji wa huduma hizi muhimu kwa maslahi mapana ya wanatanga na watanzania kwa ujumla kwa dhati kabisa mheshimiwa mkuu wa wilaya kazi kubwa na nzuri imefanyika tumeiyona na tunaamini kupitia hospitali hii sambamba na kuwasogezea wananchi huduma inayoenda kutusaidia katika utoaji wa fursa mbalimbali za ajira kwa watanzania na wasomi wetu, "alibainisha Shaib. 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Safi Medics Hospital Dkt Joseph Mberesero amesema hospitali hiyo imejikita zaidi katika utoaji wa huduma kwa kina mama na watoto ikiwemo utoaji wa kliniki kwa kinamama wajawazito,  ugumba,  na kufanya upasuaji kwa kina mama wajawazito na wasio wajawazito. 


"Kwa sasa hivi tumeongeza sehemu ya jengo letu ili kuongeza wigo watu ambao tutakuwa tunawahudumia kwani jengo hili la OPD linakuwa na kliniki mbalimbali, niishukuri serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuunga mkono sekta binafsi, "alisema Dkt Mberesero. 


Dkt. Mberesero alisema kuwa mradi huo utakapokamilika utasaidia kuimarisha huduma zaafya ngazi ya wilaya,  kutoa ajira kwa wananchi wenye taaluma za afya,  kutoa huduma za kliniki kwa kina mama wajawazito,  huduma za kliniki kwa wagonjwa wa kisukari na figo,  kutoa huduma ya usafishaji damu, pamoja na kutoa huduma ya afya ya uzazi ya upandikizaji wa mimba. 


Mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu ahilingi milioni 245 ikiwa ni fedha za mkopo kutoka benki ya NMB. 


Miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Tanga ni pamoja na mradi wa vijana Tumbilini, uzinduzi wa kisima cha maji Mwahako, uzinduzi wa Kituo cha mafuta cha Shehoza,  Shule ya Msingi Mnyanjani ufunguzi wa vyumba vya madarasa, ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika hospital ya Safi Medics, uzinduzi wa barabara ya Askari na Lumumba kata ya Ngamiani kaskazini na chanzo cha maji Mabayani ikiwa ni pamoja na zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Pande. 


Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”. Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu ni Mkoani Manyara Oktoba 14, 2023.

No comments:

Post a Comment

Pages