Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Gawio la Serikali la Sh. Bilioni 45. 5 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede (wa pili kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kushoto) wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 25 ya mafanikio ya benki hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Katikati ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba na kushoto ni Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishiu Wetu
Serikali imeahidi kuendelea kuchangia mafanikio ya Benki ya NMB ili izidi kunufaika na ufanisi wake kiutendaji ikiwemo ongezeko la gawio lake la kila mwaka kutoka taasisi hiyo kubwa kifedha nchini inapopata faida.
Azma hiyo ya Serikali imebainishwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kusisitizwa na Msajili wa Hazina, Bw Nehemiah Mchechu, kwenye kilele cha kuadhimisha miaka 25 ya mafanikio ya benki hiyo ambapo pia Serikali ilikabidhiwa rasmi gawio la TZS bilioni 45.5 kutokana na faida ya NMB ya mwaka jana.
Takwimu zilizowasilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Ruth Zaipuna, wakati wa sherehe ya maadhimisho hayo zilizofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam zinaonyesha kuwa ndani ya miaka minne ya hivi karibuni serikali imepokea kiasi cha TZS bilioni 113.2 kama gawio kutoka NMB.
Malipo jumla ya gawio kwa wanahisa wote kati ya mwaka 2019 na 2022 zilikuwa ni TZS bilioni 356.3. Kiasi hicho kingeweza kuwa kikubwa zaidi ya hapo lakini sehemu ya faida zilizopatikana imekuwa inatumika kufanya uwekezaji wa kiutendaji na kibiashara ili kuboresha ufanisi na kupata matokeo mazuri zaidi.
Serikali inasema hilo ni jambo jema na la manufaa kwa wanahisa wa NMB na maendeleo ya benki wa ujumla, na ni muhimu pia hata kwa wananchi pamoja na maslahi mapana ya kiuchumi na kijamii.
“Gawio la TZS bilioni 45.5 ambalo nimelipokea linatokana na hisa za Serikali ambazo ni asilimia 31.8. Na kama alivyoserma vizuri Msajili wa Hazina ilikuwa tupate kiasi kikubwa zaidi lakini tukasema kiasi kingine kibaki huko benki kifanye biashara na kutoa huduma kaitka sekta nyingine au kiwahudumie wananchi,”Dkt Samia alibainisha kwenye hotuba yake.
Aidha, Mkuu huyo wa nchi alisema mafanikio makubwa iliyonayo NMB na jinsi inavyolihudumia taifa ni mfano wa kuigwa wa faida za ushirika baina ya Serikali na sekta binafsi.
Dkt Samia amezitaka taasisi nyingine ambazo Serikali ina maslahi ya umiliki kuiga ufanisi wa NMB ili nazo ziweze kuchangia mapato na fedha kwa ajili ya ujenzi wa nchi na ustawi wa jamii badala ya kuwa mizigo na hasara kwa taifa.
Akiweka bayana mpango wa Serikali kuacha kuyafadhili mashirika ya aina hiyo, Dkt Samia amemuagiza Msajili wa Hazina kukamilisha zoezi la kutathimini utendaji wake ili yakufutwa yafutwe na yakusaidia basi yapewe msaada stahiki.
“Lengo la Serikali ni kuziona hizi taasisi zinakua. Leo hii tunapofurahia kupata gawio la TZS bilioni 45.5 kutokana na hisa tunazomiliki NMB, gawio letu halisi lilipaswa kuwa TZS bilioni 136.4 kwa faida waliyozalisha ya TZS bilioni 429,” Bw Mchechu alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na kwamba Serikali itapata cheki ya TZS bilioni 45.5 ambazo tayari zimelipwa hazina kiasi cha TZS bilioni 91 kimeachwa ndani ya NMB ili kiwe mtaji wa kuzalisha faida zaidi na kuisaidia benki hiyo ikue zaidi na kuongeza mafanikio yake.
Bi Zaipuna alisema moja ya mikakati waliyonayo kwa ajili ya mafanikio zaidi siku za usoni na kuendeleza kuikuza biashara yao ni kuvuka mipaka na kwenda nje ya nchi. Hata hivyo alisema hilo litafanyika kwa umakini na uangalifu mkubwa ili watakapotoka basi uwe ni uwekezaji wenye tija na faida...
“Na ili kuendelea kukuza biashara yetu, tayari tumeanza kufanya uchambuzi yakinifu na kwa uangalifu mkubwa tutajifunza kwa kuangalia fursa za kuanza kujitanua nje ya mipaka ya Tanzania, na uamuzi utafanyika mara tutakapo kamilisha uchambuzi na kuainisha fursa hizo.”
Kutokana na mafanikio iliyoyapata kwa robo karne, NMB ina kila uwezo wa kulifanikisha hilo kwani tayari ni benki ya viwango vya kimataifa ikiwa ni ya tatu Afrika Mashariki, Pia NMB ni moja ya vigogo wa ufanisi miongoni mwa mabenki ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara baada ya kufikia uwiano wa Matumizi yasiyo ya Riba na Mapato Ghafi (CIR) wa asilimia 42.
Mbali na msuli wa kifedha kutokana na ukubwa wa mizania ambao Mwenyekiti wa Bodi, Dr Edwin Mhede, amesema mwezi huu umefikia zaidi ya TZS trilioni 11 kutoka TZS trilioni 10.2 Disemba mwaka 2022, ni ubunifu wa timu za benki hiyo.
Hati fungani ya Jasiri iliyomsisimua Dkt Samia ni kielelezo kizuri cha ubunifu wa aina hiyo. Si tu kwamba dhamana ya muda mrefu ya Jasiri ni ya kwanza upande huu wa dunia bali pia tayari imeshinda tuzo za kimataifa na inauzwa kwenye moja ya masoko makubwa ya hisa huko Ulaya.
Ni mafanikio kama haya yanayoliheshimisha taifa yaliyomfanya Makamu wa Raisi, Dkt Philip Mpango, kuiita NMB fahari ya Watanzania bila kusita wakati anaizungumzia safari yake ya mafanikio miaka 25.
No comments:
Post a Comment