HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2023

Wellworth wanavyotafsiri Royal Tour kivitendo


Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akikata utepe wakati wa uzinduzi wa hoteli ya kitalii ya Ngorongoro Oldeani Moutain Lodge iliyopo wilayani Karatu mkoani Arusha, wengine ni Mwenyekiti wa Wellworth Ismail Gulam, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella, Mama Mpango na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa.


Na Selemani Msuya

 

TANZANIA imejaaliwa maeneo ya hifadhi za wanyamapori, misitu na nyuki ambavyo kwa pamnoja vinaifanya sekta ya maliasili na utalii nchini kuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa na fedha za kiugeni.

 

 Kiuchumi, maliasili na malikale zimeendelea kuchangia katika kuingiza fedha za kigeni na Pato la Taifa (GDP) kupitia utalii, ajira, nishati, elimu, utafiti, utamaduni, burudani na tiba. 

 

Takwimu zinaonesha sekta ya utalii huchangia takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni na zaidi ya asilimia 17 katika Pato la Taifa. 

 

Mchango wa sekta hiyo umekuwa ukishajihishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo imepewa dhamana ya kusimamia uhifadhi wa maliasili, malikale na maendeleo ya utalii. 

 

Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, mipango ya maendeleo na maelekezo mbalimbali ya Serikali.

 

Maeneo ambayo yameweza kuchangia sekta ya utalii kuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa ni hifadhi kama Ngorongoro, Manyara, Tarangire, Kilimanjaro, Mikumi, Ruaha, Serengeti, Burigi, Mkoamazi na nyingine nyingi.

 

Moja ya hifadhi ambayo inatajwa kufanya vizuri ni Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambayo ndani yake utakutana na Bonde la Ufa, Olduvai Gorge, wanyama wa kila aina, milima na mengine mengi.

 

Pia ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kuna hoteli na lodge nyingi nzuri na za kuvutia ambazo hupokea wageni kutoka pande mbalimbali duniani.

 

Hoteli na lodge hizo zipo hadi maeneo ya nje ya hifadhi kama Karatu, Serengeti, Babati na kwingineko ambapo wageni wanazitumia kufikia na kupumzika baada ya kutembelea eneo la hifadhi.

 

Taarifa zinadai kuwa hoteli na lodge hizo kutokana na uzuri na utulivu uliopo hata watu wenye  mikutano ambayo inahitaji utulivu ewa hali ya juu wamekuwa wakizitumia.

 

Wingi wa hoteli na lodge zilizipo katika eneo linalozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro unatajwa kuwa bado haukidhi mahitaji ya wageni wanaokuja kufanya utalii nchini.

 

Juni 9, 2023 wakati akifungua mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan aliwahimiza watu wa sekta binafsi kuchangamkia fursa ya kujenga hoteli za kitalii kwa ajili ya watalii, kutokana na ongezeko la wageni ambalo limeanza kuonekana.

 

Rais Samia alitumia jukwaa hilo kuwataka wasaidizi wake kupunguza vikwazo katika kutoa vibali vya ujenzi wa hoteli ili kazi ziende kwa haraka na watalii wakija wasikutane na changamoto ya mahali pa kufikia.

 

Msisitizo wa Rais Samia katika kuweka mazingira rafiki kwenye sekta ya utalii, unatokana na kampeni aliyoifanya kupitia Royal Tour ambapo taarifa zinaonesha kuwa imeanza kuzaa matunda.

 

Katika kampeni hiyo Rais Samia alishiriki kuandaa Filamu ya Royal Tour kwa kuonesha maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii ambayo Tanzania imejaliwa.

 

Baadhi ya maeneo ambayo kiongozi huyo wa nchi alipita na kuonekana katika filamu hiyo ni Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro katika eneo la Bonde la Ufa.

 

Msisitizo huo wa Rais Samia kushawishi wawekezaji katika sekta ya utalii, umeungwa mkono na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ambapo wakati akizindua hoteli ya nyota tano ya Ngorongoro Oldeani Mountain Lodge ambapo aliwaomba wawekezaji wazawa na wageni kuwekeza katika sekta hiyo.

 

Makamu wa Rais alisema asilimia 17 ya mchango wa sekta ya utalii kwenye pato la taifa inaweza kuongezeka iwapo kutakuwa na uwekezaji mkubwa.

 

“Wellworth wameonesha mfano kwa kujenga hoteli ya kisasa, nitumie nafasi hii kuwaomba Watanzania na wageni kushiriki katika sekta hii kwani inalipa. Rais Samia ameitangaza vivutio vyetu kwa nguvu sana tunatarajia wageni wataongezeka,” alisema.

 

Makamu wa Rais amewapongeza wamiliki wa hoteli hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha utalii kwa kujenga miundombinu ya hoteli katika eneo la Karatu lenye idadi kubwa ya watalii. 

 

Pia amewapongeza wamiliki wa hoteli hiyo kwa kutoa ajira kwa watanzania na kuwajali kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya hoteli hiyo.

 

Makamu wa Rais amewaasa vijana wanaopata nafasi kufanya kazi katika hoteli za kitalii kuendelea kuwa waaminifu na mfano katika jamii kwa kuwa waadilifu na wachapakazi kila wanapopata fursa.

 

Aidha ametoa wito kwa wadau hao wa utalii kuendelea kushirikiana na jamii ikiwemo kuwasaidia wafugaji kuhakikisha wanafanya ufugaji wenye tija katika maeneo yao. 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Wellworth, Zulfikar Ismail anasema wamewekeza katika ujenzi wa mahoteli ya kisasa, ili kuweza kuvutia watalii kutoka pande zote za dunia na Mkoa wa Arusha ni mojawapo ya maeneo muhimu kwao.

 

Ismail anasema ujenzi wa Ngorongoro Oldeani Mountain Lodge umezingatia vigezo vya kimataifa vya hoteli ya nyota tano, hivyo kuwataka wageni kufika ili wanufaike na huduma zao.

 

Anasema Ngorongoro Oldeani Mountain Lodge ipo umbali wa kilomita 15 kutoka hifadhi ya Ngorongoro, hivyo kuwaomba wageni kufikia hapo ili wafaidi mazuri ya hifadhi.

 

“Sisi tumewekeza katika hoteli takribani 22 ikiwemo Ngorongoro, Oldeani Mountain Lodge, Lake Manyara Kilimamoja Lodge, Tarangire Kuro Treetops Lodge, Kunduchi Wet n Wild Waterpark,Ole Serai Luxury Camp na nyingine nyingi. Lengo pamoja na kuchangia pato la taifa, lakini pia tunamuunga mkono Rais Samia kwenye kampeni ya Royal Tour,” anasema.

 

Ismail anasema katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kukuza utalii, wanaendelea na maboresho ya Kunduchi Beach Hotel na Zanzibar Beach Resort.

 

Anasema pia wanajenga hoteli mpya za Serengeti Lake Magadi Lodge, Mikumi Wildlife Lodge na Zanzibar Whispering Palms.

 

“Tumejipanga kuunga mkono Serikali, hivyo tunatarajia kujenga hoteli zingine zaidi ya sita ikiwemo The New Embassy Hotel, The New Hotel Agip, Tarangire Lakeview Logde, Ngorongoro Lake Masek/Ndutu, Serengeti Gurumeti Lodge na nyingine,” anasema.

 

Mkurugenzi huyo anasema kwa sasa hoteli zinazofanya kazi zimetoa ajira zaidi ya 500 huku asilimia kubwa wakiwa watanzania, jambo ambalo linaonesha dhamira yao ya kumkomboa mwananchi.

 

Anasema ujenzi wa hoteli zote ambazo zipo chini yao ukikamilika wataweza kuajiri zaidi ya watanzania 1,000 hali ambayo inaongeza mchango kwenye pato ya taifa.

 

Ismail anasema hadi sasa Wellworth  imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 400 katika ujenzi wa hoteli za kitalii na kwamba Ngorongoro Oldeani Mountain Lodge pekee zaidi ya shilingi bilioni 12 zimetumika hadi kukamilika kwake.

 

“Tunachofanya kwa sasa ni kutafsiri maelekezo ya Rais Samia kivitendo, ili dhamira yake ya Royal Tour iweze kutimia, haturudi nyuma, tunachotaka ni wasaidizi wake watupe ushirikiano tutajenga hoteli zenye hadhi ya Ngorongoro Oldeani Moutain Lodge nyingi,” anasema.

 

Meneja Operesheni wa Ngorongoro Oldeani Moutain Lodge, Vedastus Willy anasema ubora wa hoteli hiyo umekuwa kivutio kikubwa kwa wageni kwa kuwa ipo karibu na Bonde la Ufa.

 

Anasema lodge hiyo imezungukwa na miti ya asili, hivyo kuvutia ndege wengi, hali ambayo inamfanya mgeni aone yupo katika hifadhi, hata kabla hajaenda hifadhini.

 

“Pia kuna huduma bora za vyakula na vinywaji, michezo ya wakubwa na watoto, mazoezi, masaji, eneo la kujisomea.

 

Hapa tuna vyumba 51 na chumba kimojakina hadhi ya kiheshima hata kulala Rais, lakini vyumba 50 vilivyobakia vina sifa za kimataifa,” anasema.

 

Willy anasema wanapokea wageni wengi kutoka nchi za Ulaya, Marekani na Asia.

 

Anasema jambo kubwa ambalo wanajivunia ni kuweza kutumia umeme wa jua katika vyumba vyote 51, hali ambayo inachangia utunzaji wa mazingira.

 

Meneja huyo anasema hoteli hiyo imeweza kuchangia ajira kwa watanzania kwa asilimia 95 na wengi wakiwa ni wanaotoka katika wilaya ya Karatu.

 

“Tunachokifanya hapa ni kuunga mkono Kampeni ya Royal Tour inayoongozwa na Rais Samia, kwani wageni wamekuwa wakimiminika kila siku,” anasema.

 

Willy anasema eneo hilo linapakana na Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, kijiji cha Wahzabe, Hifadhi ya Manyara na Tarangire, hivyo ni imani yao kuwa watachangia ukuaji wa uchumi kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

Pages