HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 07, 2023

CHUO KIKUU MZUMBE: WATANZANIA NJOONI SABASABA

Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (kushoto) akipata maelezo kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho alipotembelea banda hilo katika Maonyesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) leo Julai 7, 2023.





 

Na Mwandishi Wetu

CHUO Kikuu Mzumbe kimetoa wito kwa Watanzania kutembelea Banda lao  katika maonesho ya kimataifa ya Sabasaba, kujionea bunifu na mambo mbalimbali yanayoendeshwa na Chuo hicho.

Hayo yamebainishwa leo Julai 7, 2023 bandani hapo na Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha ambapo amewataka watanzania na wadau mbalimbali wa elimu kufika kujifunza Programu zao na kujua kozi zinzotolewa na Chuo hicho.

"Nichukue nafasi hii kuwakaribisha kwenye Banda letu la Chuo Kikuu Mzumbe ambapo mwaka huu tumejipanga kuja kuonyesha mambo ambayo tunayafanya. Kwanza kazi zetu Kuu ambazo tunazifanya ni eneo la ufundishaji ambapo tumekuja kuonyesha mifumo yetu ya Elimu kwa upande wa Shahada ya Udhamili na Udhamivu pamoja na kozi mbalimbali za Shahada, Astashahada na Stashahada.  

"Kazi yetu kubwa ni kuelimisha jamii wafahamu kozi zetu ili waje kusoma Mzumbe, tumejipanga kuelimisha na kutoa msaada kwa wale ambao wanakuja kwa ajili ya kupata udahili." Amesema na kuongeza kuwa.

"Labda niseme tu kwamba, Programu zetu ni nzuri, tunatoa elimu ambayo inawaandaa vijana wetu ama wahitimu wetu kuja kupambana na changamoto za maisha kwenye soko la ajira lakini pia kujiajiri wenyewe.  


"Nichukue nafasi hii kuwatia moyo wale ambao wanahitaji kuja, waje wajielimishe kwenye Banda letu lakini pia wapate nafasi ya kufanya udahili katika Chuo chetu." Ameongeza kuwa.


"Eneo lingine ambalo tunaliangalia kuja kulionyesha hapa kwenye Banda letu la Mzumbe ni shughuli yetu ya utafiti, tunafanya tafiti mbalimbali, kiukweli tunalenga tafiti ambazo zinakuja kujibu maswali ya changamoto ambazo tunazo kama Jamii ya  Watanzania lakini pia kama raia wa Dunia.


 "Tafiti zetu nyingi zimelenga kusapoti mifumo ya afya, lakini pia kuangalia mambo ya biashara, upande wa menejimenti na utawala ambayo ni ya msingi. Sisi Chuo Kikuu Mzumbe tuna kauli mbili yetu ya ' Chuo Kikuu Mzumbe tujifunze kwa maendeleo ya watu' ndio maana tunalenga kwenye sekta ambazo zinaenda kuchochea maendeleo katika jamii." Amesema huku  akisisitiza kuwa.


"Maeneo mengine ambayo ni muhimu tumekuja kuonyesha hapa ni upande wa kozi fupi, tunatoa kozi fupi nyingi sana kwa ajili ya kujenga uwezo, sio tu kwa watumishi wa Serikali lakini pia wajasiriamali wa kada zote, kwenye Banda letu tuna eneo maalumu ambalo watu watakuja kuzifahamu hizo kozi." Amesema.

Hata hivyo amebainisha kuwa wanaonyesha pia bunifu mbalimbali ambazo zinafanywa na wanafunzi wao ambao wamewawekea kitengo maalumu cha kuziendeleza bunifu hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages