Na Khadija Kalili
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo leo Jumamosi Julai 15, 2023 ametoa agizo kwa Jiji la Dar es Salaam kuipa kibali Kampuni ya kuchakata na kudhibiti taka ya Givorah Recycling Limited cha kuchukua takataka katika dampo la Pugu Kinyamwezi ambalo linamilikiwa na halmashauri ya Jiji hilo.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo wakati akizindua kiwanda hiko kilichopo Kata ya Mtoni Wlayani Temeke Jiini Dar es Salaam mara baada ya kupokea changamoto iliyowasilishwa kwake kwamba Kiwanda hiko ufanisi wake unazuiwa na upatikanaji wa malighafi taka ambazo wanapokwenda kuchukua katika sehemu zinapopatikana hususani katika dampo la Pugu Kinyamwezi huombwa kibali ili hali wao wanasaidia katika uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa taka.
Dkt. Jafo amesema kuwa, Givorah Recycling Limited ni miongoni mwa Kampuni ambazo zimetekeleza sheria za nchi , na kukikidhi vigezo vya mazingira hatua ambayo imewawezesha kupata cheti cha mazingira (Environmental Certificate) kinachotolewa na Ofisi yake.
Waziri Jafo amesema kuwa Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla wake linazalisha taka kati ya tani 6,000 hadi 7,000 kwa siku hivyo ujio wa Kampuni ya Givorah ni msaada mkubwa karika kudhibi uchafuzi wa mazingira Jijini Dar es Salaam lakini badala yake ameshangazwa kuambiwa Kampuni hiyo changamoto yake kubwa ni upatikanaji wa malighafi taka na kuzuiwa kuchukua taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi.
"Jiji la Dar es Salaam linazalisha taka kati ya tani 6,000 hadi 7,000 kwa siku, na Jiji la Dar es Salaam niseme ukweli hatuna dampo la kisasa lakini cha ajabu kiwanda cha kuchakata na kudhibiti taka cha Givorah changamoto yake kubwa ni kupata taka kama malighafi" amesema kwa mshangao Waziri Jafo na kuongeza
"Nafahamu lile dampo la Pugu Kinyamwezi lipo katika umiliki wa Jiji la Dar es Salaam, nilichosikia ni kwamba Kampuni ya kuchakata na kudhibiti taka ya Givorah Recycling Limited inahangaikia kupata vibali vya kuruhusiwa kuchukua taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi ni maajabu sana, yaani kuna watu wanataka kutusaidia kuchukua taka lakini kibali cha kuchukua taka hakitoki"amesema Waziri Jafo.
Aidha Waziri Jafo ametoa agizo kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ifikapo Julai 30, mwaka huu Kampuni ya Givorah Recycling Limited iwe imepata kibali hiki siyo ombi bali ni amri.
Wakati huohuo Waziri Jafo ametoa rai kwa Kampuni hiyo kuwa na vihifadhi taka (dust bin) katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Taasisi za serikali kama mashuleni, Hospitalini, Sokoni na kwenye mitaa mbalimbali na kwa kuanzia waanze na Wilaya ya Temeke baadaye wasambaze vifaa hivyo katika maeneo ya Dar es Salaam kwa sababu itawarahisishia kupata malighafi wanayohitaji kwa ajili ya uzalishaji.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Givorah Recycling Limited , Mwanasheria wa Kampuni hiyo Wakili Shehzada Walli amesema kuwa, Kampuni hiyo imeweza kukusanya asilimia 30 ya taka zilizozalishwa katika kipindi cha Maonesho ya Biashara (Sabasaba) mwaka huu na kuongeza kuwa kama siyo wao kukusanya taka hizo zingekweda dampo na hata kuchafua mazingira.
Wakili Walli amesema kuwa, changamoto yao kuu wanayopata ambayo pia ni ya kushangaza ni kwamba badala ya jamii kuisaidia Kampuni kukusanya taka bure wao wanataka kuuza taka zao jambo linalopelekea Kampuni kupata shida inapokwenda kukusanya taka na kupunguza ufanisi katika uzalishaji.
Kufuatia hilo Wakili Walli ameiomba serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira iwasaidie kutoa elimu kwa wananchi kwamba Kampuni yao inatoa mchango katika kulinda na kusafisha mazingira na hivyo wawaunge mkono na kuwapa ushirikiano.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya amesema kwa siku moja taka zinazozalishwa ndani ya manispaa hiyo ni tani 1,400, taka zinazotolewa kwa siku ni tani 964 huku taka ambazo hazipati udhibiti kabisa kwa siku ni tani 379.
Mabelya amesema kuwa, na dampo wanalolitegemea la Pugu Kinyamwezi limezidiwa na hivyo ujio wa kampuni ya Givorah Recycling Limited imekuwa ni mkombozi katika Halmashauri yetu ya Temeke huku akiahidi kushirikiana bega kwa bega na Kampuni hiyo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Abdallah Mtinika amesema kuwa ujio wa Kampuni ya Givorah Recycling Limited ni neema na faida kwa wana Temeke huku akitoa ahadi ya kuwalinda na kushirikiana nao katika utendaji kazi wao wa kila siku na kwamba watakuwa wanawatembelea mara kwa mara ili kuwasikiliza changamoto zao na kujua mwenendo wao katika uzalishaji.
Mtinika ameongeza kuwa, Miji mingi iliyofanikiwa Duniani na kuonekana inapendeza jambo hilo linatokana na mambo mawili makubwa ambayo ni usimamizi thabiti wa usafi na udhibiti wa taka miongoni mwa jamii.
Givorah Recycling Limited ni Kampuni inayojishughulisha na ukusanyaji na udhibiti wa taka zote ambazo zinazoweza kutumika tena ikiwa na uwezo wa kuzichakata (recycle) taka hadi tani 1,000 kwa siku.
Kampuni hiyo ambayo ilianzishwa nchini India ipo pia katika nchi za Marekani, Ulaya, Falme za Kiarabu na mwaka huu imeanzishwa rasmi nchini Tanzania.
Wakati huohuo Mheshimiwa Jafo amevipongeza vyombo vya habari kutokana na mchango wake mkubwa wa kuandika habari mbalimbali zinazohusu utunzaji wa mazingira nchini na hivi sasa wachuuzi wa miti wametapakaa pembezoni mwa barabara wakiuza miti badala ya kuuza machungwa elimu mliyoitoa kwa jamii imezaa matunda na yanaonekana.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Mobhare Matinyi ambaye ana udhuru.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Abdalah Mtinika na Mheshimiwa Diwani wa Mtoni Amina Abdullah Batash.
No comments:
Post a Comment