HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 12, 2023

MSAMALA WATAMBULISHA UJENZI WA SEKONDARI YA DKT DAMAS NDUMBARO

 NA STEPHANO MANGO, SONGEA

 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wamepokea jumla ya shilingi mikioni 560.5 kutoka Serikali kuu kwa ajiri ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Dkt Damas Ndumbaro ambayo itajengwa Mtaa wa Mtaungwana katika kata ya Msamala.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa kata hiyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Maiko Mbano alisema kuwa ujenzi wa sekondari hiyo utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wazazi na wanafunzi wa kata hiyo na maeneo jirani.

 

Mbano alisema kuwa kwa muda mrefu wananchi wa eneo hilo walikuwa na kilio kikubwa sana kwani watoto wao walikuwa wanaamka usiku na kujiandaa kwenda kusoma shule iliyopo zaidi ya kilometa nane ambapo kwenda na kurudi wanafunzi wanatembea jumla ya umbali wa kilometa 16.

 

“Kitendo hicho cha wanafunzi kutembea umbali mrefu huku wakiwa wamebeba mabegi mgongoni ya madaftari ni ukatili mkubwa kwasababu muda mwingi wamekuwa wakiteseka barabarani kutembea na wakati mwingine wamekuwa  wakikumbana na  vishawishi mbalimbali vya kufanya vitendo viovu” Alisema Mbano.

 

Mbano ambaye pia ni Diwani wa kata hiyo ya Msamala alisema kuwa Wananchi wa kata hiyo wanatakiwa kumshukuru na kumuombea sana Rais Dkt Samia Hassan Suluhu na Mbunge wa  Jimbo la Songea Mjini Dkt Damas Ndumbaro kwa kuwaletea fedha za kutekeleza mradi huo ambao utaondoka kero na kukuza ufaulu kwa wanafunzi.

 

Alisema kuwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kata hiyo imepokea Zaidi ya shilingi bilioni 1.3 ambapo Zaidi ya milioni 700 zimepelekwa kwenye shule ya Dkt Emmanuel Nchimbi kwenda kuongeza miundombinu kwa ajiri ya kuwapokea wanafunzi 500 wa kidato cha tano mwaka huu.

 

Akizungumza  kwenye mkutano huo Afisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo John Ngairo alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuwachagua wajumbe wazuri wa kamati ambazo zitahusika na ujenzi wa shule hiyo mpya.

 

Ngairo alisema kuwa wajumbe wa Kamati za Utekelezaji na Mapokezi ya vifaa vya ujenzi wanatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na uwazi kwani Shule hii ni ya wananchi hivyo wanatakiwa kuwa wazalendo wa hali ya juu.

 

“Ili mradi huo ukamilike kama unavyotarajiwa suala la manunuzi linatakiwa liangaliwe sana, pamoja na ubora wa vitu vitakavyonunuliwa, kwani manunuzi yakichezewa mradi huo hautakamilika kwa wakati na hakutakuwa na fedha za kuongeza katika utekelezaji wa mradi”alisema Ngairo.

 

Aidha katika kikao hicho wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri walitoa maelekezo na miongozo mbalimbali ya namna ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia Sheria taratibu na Kanuni za manunuzi, ikiwa Ni pamoja na kuunda Kamati mbalimbali zitakazosimamia utekelezaji wa mradi huo.

 

Naye Afisa Elimu wa halmashauri hiyo Janeth Moyo alisema kuwa fedha hizo ambazo zimeletwa na Serikali zitawezesha kujenga vyumba vya madarasa nane, matundu 20 ya vyoo, maabara ya kemia,fizikia na baiolojia.

 

Moyo alisema kuwa wananchi wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika majitoleo ya kusafisha eneo la mradi, kuchimba msingi na kuchotelea maji na kazi zingine ndogo ndogo kwani kazi hizo hazitalipwa kulingana na maelekezo ya mradi

MWISHO

No comments:

Post a Comment

Pages