Na Mashaka Mhando Tanga
CHAMA Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga, kimemaliza mgogoro wa madiwani wa halmashauri ya mji wa Handeni, kukataa bati zilizoletwa kwa ajili ya kuezeka katika shule zao wakidai hazina ubora.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Ustadh Rajab Abrahaman Abdalah akizungumza baada na madiwani pamoja na viongzozi wa wilaya hiyo, alisema mzabuni aliyeleta bati hizo arejeshe fedha za serikali kutokana na kuidanganya serikali kwa kuleta bati zisizokuwa na kiwango.
Shirika la Viwango nchni TBS walileta majibu kwamba bati hizo hazina viwango vinavyotakiwa baada ya kupelekewa sampuli na kisha kufika wilaya ya Handeni ambako TBS walichunguza na kuzipima bati mbalimbali zilizoletwa na kampuni hiyo.
"Kwa hili lililofanyika CCM inatoa maelekezo kwamba kampuni iliyoleta mabati hayo irudishe fedha walizolipwa lakini pia serikali ikanunue bati kwingine ambako bati zake zitakuwa za viwango.
Awali mkuu wa wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando alipopokea malalamiko alielekeza bati hizo zikapimwe na endapo zitakuwa feki mkandarasi alete nyingine zitakazokubalika.
Mkuu wa wilaya hiyo katika taarifa yake aliyoitoa jana alisema kumekuwa na sintofahamu kuhusu bati zilizosambazwa na kampuni ya Great City Material Tanzania Limited ya Jijini Arusha.
Alisema anawashukuru na kuwapongeza wote ambao wanafuatilia na kusimamia miradi inayotekelezwa na serikali na kuona kasoro mbalimbali.
"Nawapongeza Wahe. Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mji Mussa Abeid Mkombati kwa kukagua na kutoa taarifa kuhusu ubora wa bati zilizosambazwa na kampuni ya Great City Material Tanzania Limited," alisema.
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo Ofisi yake imechukua hatua ambapo Julai 2, 2023 alifika na kuona bati hizo ambapo alielekeza kuchukuliwa kwa sampuli za mabati hayo zikapimwe na TBS ili kuthibitisha ubora kama ambavyo Kamati ya Fedha ya Madiwani ilishauri.
Hivyo aliwaomba wote wawe na subira ili kukamilisha zoezi hilo na endapo itathibitika hazina ubora watahakikisha Mzabuni anawajibika na bati hizo hazitatumika.
Alisema kwa kuwa Mzabuni alitoa warranty ya miaka mitano itamlazimu kubeba gharama zote za kubadilisha bati hizo na ikithibitika zina ubora Mafundi wataendelea na ujenzi kama kawaida.
Awali wakizungumza na Habari Mseto baadhi ya madwani ambao hawakutaka majina yao yatajwe walilalamika utaratibu uliotumika kununua mabati hayo.
Diwani mmoja alisema ofisi ya mkuu wa wilaya ndiyo iliyohusika kumtafuta mzabuni ambaye ndiye aliyeleta mabati hayo yanayodaiwa kuwa hayana ubora.
Diwani mwingine alisema kuwa wapo wazabuni katika wilaya ya Handeni ambao mara nyingi wamekuwa wakiwatumia katika miradi mbalimbali wangepewa zabuni hiyo wangeleta mabati kutoka kiwandani kwa bei tofauti na yaliyonunuliwa.
"Watu wa TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) wanatakiwa jambo hili walichunguze kwa makini sana haiwezekani ununue mabati kutoka kiwandani kwa bei ile," alisema.
Mabati hayo yamenunuliwa kwa bei ya Sh 43,700 kiwandani Mkoani Arusha kwa kila moja na yapo zaidi ya 2,000 katika halmashauri hiyo na mengine zaidi ya hayo yamepelekwa halmashauri ya wilaya ya Handeni.
Pia madiwani hao walidai kuwa wamekuta kasoro katika misumari mfuko wa kilomoja wamekuta robokilo hamna.
No comments:
Post a Comment