HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 09, 2023

Ruzuku kunufaisha wakulima wadogo nchini


Oswald Jackson mkulima wa maharage akikagua shamba lake katika kijiji cha Matanga, Sumbawanga. Picha na Hamis Adam.

 

NA MIKE MANDE

 

Wakulima wadogo zaidi ya 100,000 kutoka mikoa 11 ya Tanzania Bara watanufaika na ruzuku ya Shilingi Bilioni 5 kuendeleza zao la alizeti, maharage na mbaazi katika msimu huu wa kilimo.

 

Mikoa itakayofaidika na ruzuku hiyo iliyotolewa na nchi za Denmark and Sweden ni pamoja na Manyara, Singida, Dodoma, Lindi, Njombe, Ruvuma, Mtwara, Songwe, Rukwa , Iringa na Dar Es Salaam.

 

Charles Ogutu, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya Masoko ya Kilimo (AMDT) amesema kuwa ruzuku hiyo itawezesha upatikanaji wa mbegu bora ambapo kilo 100,000 za alizeti zitazalishwa ili kutumika katika ekari 50,000 msimu huu.

 

Ogutu alisema ruzuku hiyo pia itawezesha upatikanaji wa huduma za biashara na fedha katika mnyororo wa mazao hayo na kuboresha huduma za ugani, usimamizi wa mavuno na uchakataji wa mazao hayo ili kuongeza thamani.

 

“Miradi itakayopambana vizuri kwa mafanikio makubwa itaongezwa nguvu na muda wa utekelezaji mpaka mwaka 2024. Miradi yote itazingatia mafunzo na uhamasishaji wa mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa lengo la kujenga ustahimilivu kwa wakulima”, alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages