HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 30, 2023

Usahihi wa utabiri mvua za masika ni asilimia 86.4


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a akizungumzia viwango vya usahihi wa taarifa za msimu wa Masika mwaka 2023.

 

Na Irene Mark

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeendelea kujivunia usahihi wa viwango vya utabiri wake baada ya viwango hivyo kufikia asilimia 86.4 kwa utabiri wa mvua za Masika, 2023.

Utabiri wa mvua za Masika zinazoanza Machi, Aprili na Mei (MAM), kila mwaka ulitolewa Februari 22,2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), usahihi wa viwango vya utabiri ni asilimia 70 na zaidi hali ambayo TMA imepitiliza kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Akizungumzia ubora wa viwango hivyo, Dk. Chang’a alisema ni kutokana na ubora wa vifaa kazi na wataalam wenye weledi wanaotoa na kupokea taarifa kila wakati.

"Kwenye hili tuna kila sababu ya kuishukuru serikali maana imetuwezesha kupata rada saba na kompyuta ya kisasa zaidi yenye uwezo wa kuchakata taarifa zetu kwa haraka.

"Usahihi wa taarifa hizo ni matokeo ya ufuatiliaji makini wa viashiria vya utabiri, wataalam na vitendea kazi vya kisasa," alisema Dk. Chang'a.

Alisema serikali inaendelea kuijengea uwezo TMA na kuimarisha huduma zake ikiwemo utoaji wa taarifa za hali ya hewa kila wakati na kuwafikia watumiaji ambao huzipata kwa usahihi na kuzitumia.

"Kwa sababu hii tunawaomba waandishi wa habari tuendelee kushirikiana ili taarifa zetu sahihi zifike kwa watumiaji wa taarifa zetu na wataalam mbalimbali wa maafa, kilimo, afya na wananchi wote," alisisitiza Dk. Chang'a.



No comments:

Post a Comment

Pages