*Yageuka kimbilio kwa wenye vipato tofauti, faida sasa Trilioni 1.5/-
Na Beatrice Sanga-MAELEZO
KAMPUNI ya Uwekezaji wa Mitaji ya Pamoja (UTT AMIS) imetoa rai kwa wananchi kuwekeza kwenye mifumo mbalimbali ya kampuni hiyo ili kuweza kujikimu kimaisha na kuwa na uhakika wa maisha ya sasa na ya baadae ambapo kwa sasa inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu uwekezaji huo na kwamba imekuwa kimbilio la wengi bila kujali vipato vyao.
Hayo yamebainishwa Julai 31, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Msajili wa Hazina, UTT AMIS, Wahariri na waandishi wa habari wenye malengo ya kuelezea majukumu na namna gani kampuni hiyo inafanya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala amebainisha kuwa majukumu yao ni kuboresha huduma na faida kwa wawekezaji wadogo na wakubwa wa Kampuni hiyo ili kuvutia uwekezaji.
"UTT tunakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo watu wengi kukosa uelewa na elimu ya masoko ya fedha pia watu wengi hawana kipato kikubwa cha kuwekeza tumezingatia shida zetu kuliko kuwekeza tunahitaji kuwekeza kwa malengo ya baadae," amesema Migangala.
Aidha, Migangala amebainisha kuwa huo ni mwendelezo wa uelimishaji kuhusu majukumu yanayofanywa na Kampuni hiyo ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wote bila kuangalia kipato chao.
Amesema mifuko ya UTT AMIS imeboreshwa kwa uwekezaji wenye malengo ya muda mrefu na muda mfupi ili kuhakikisha kila mtanzania anawekeza kwa maslahi yake na taifa kwa ujumla.
"Maisha yetu Tunategemea fedha, ikiwa tofauti na miaka ya zamani kwa wengi tulikuwa tunarithishwa ardhi, lakini sasa hivi urithi wetu unategemea kwenye uwekezaji wa fedha hivyo niwahimize kuwekeza UTT AMIS, kwani kila mtanzania atajivunia," amesema Migangala.
Akizungumzia mafanikio ya miaka minne mfululizo waliyopata kutokana na uwekezaji mdogo na mkubwa, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Kampuni hiyo imeweza kuchangia katika Pato la Taifa na kutoa gawio kwa kila mwaka kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina.
"Mafanikio haya ni kwa mwaka juzi 2021 ukuaji wa Taasisi kutoka bilioni 600 hadi bilioni 996 sawa na asilimia 50 kwa mwaka 2022 kutoka bilioni 996 hadi trilioni 1. 5 sawa na asilimia 54 ukuaji huu umeenda vizuri ikiwa ni tofauti na miaka ya nyuma," amefafanua Migangala
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambao ulianza Julai mwaka huu ukuaji umeongezeka hadi kufikia asilimia 12 na kuweza kuchangia kwenye pato la Taifa kwa miaka sita mfululizo.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kuwekeza kwa sababu Kampuni hiyo iko imara kwani kuwekeza ni fursa kwa mwekezaji mdogo na mkubwa wanapata faida sawa.
Kwa upande wake Angela Akilimali ambaye ni Mjumbe Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) amesema kuwa UTT AMIS inatakiwa kuendelea kuelimisha jamii kuhakikisha kuwa wananchi wanachangamkia fursa ya uwekezaji katika mfuko huo.
“Timu hii iko imara inawakilisha waandishi wengine ambao hawajafika hapa na tutahakikisha ujumbe wenu unafika na watu wanaitambua UTT AMIS, Taasisi ambayo ni nzuri ya uwekezaji lakini wengine wanashindwa kufahamu, nina imani hii elimu ambayo tumeipata hapa imetufafanulia zaidi kwamba hata mtu wa hali ya chini anaweza kuwekeza katika masuala ya UTT AMIS, huko mtaani watu wana mawazo mengi, wanakuwa hawaelewi wapi waende ili kuwekeza kwa ajili ya watoto wao.” Amesema Akilimali.
Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea na utaratibu wake wa kukutanisha Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya ofisi hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi ambapo leo Kampuni ya UTTM AMIS imepata nafasi na kuzungumzai mafanikio yao na mwelekeo wao.
No comments:
Post a Comment