HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 22, 2023

SERIKALI YAFURAHISHWA HUDUMA ZA SOS CHILDREN’S VILLAGE


Rais wa Dunia wa SOS Children's Village akisalimiana na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ally alipomtembelea ofsni kwake Dar es Salaam.

 

NA MWANDISHI WETU, DAR


SERIKALI imeahidi kuendeleza ushirikiano na Taasisi ya Kimataifa ya SOS Children’s Village kwa kutoa huduma zinazolenga kuimarisha ustawi wa watoto, vijana, familia na jamii kwa ujumla.

 

Pia serikali imepongeza shirika hilo kwa kuongeza wigo wa huduma kutoka zile za kuhudumia watoto kwenye makao hadi kushiriki kwa kutoa mchango wa kitaalamu na fedha kwenye uandaaji wa Sheria, Kanuni na  miongozo mbalimbali ya huduma za Ustawi wa Jamii nchini.

 

Ahadi hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Ally wakati akimkaribisha Rais wa SOS Children’s Duniani, Dereje Wordofa aliyemtembelea ofisi ndogo ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam juzi Septemba 19. 2023. 

 

Alisema shirika la SOS Children’s Villages limekuwa mdau mkubwa wa serikali katika utekelezaji wa miongozo ya uimarishaji wa mifumo na utoaji wa huduma kwa watoto na familia zilizo katika mazingira hatarishi hususan watoto na familia zilizo katika mikoa wa Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Zanzibar na maeneo mengine ya nchi.

 

“Aidha, ninawapongeza kwa kubuni miradi inayoakisi matakwa ya mifumo ya serikali ya ulinzi na usalama wa mtoto hususan mifumo ya Malezi mbadala na huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi.

 

Miradi kama ile ya Malezi mbadala, mradi wa kuimarisha familia, mradi wa Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, mradi wa kuunganisha watoto na familia, mradi wa uchechemuzi, mradi wa uvumbuzi upya Arusha pamoja na mradi wa Watoto wenye Watoto - Iringa (Children with Children) ni miradi mizuri ya kutolea mfano”alisema naibu waziri huyo.

 

Aidha Mwanaidi alisema Serikali inatambua ushirikiano wa dhati kati ya SOS Children’s Villages na Wizara yake  katika masuala mtambuka ikiwa ni pamoja na kutoa mchango wa utaalamu na fedha katika kufanikisha masuala mbalimbali yakiwemo naya kisera.

 

Aliitaja baadhi ya michango hiyo kuwa ni pamoja na mchakato wa uandaaji wa Sheria ya Watoa Huduma za Ustawi wa Jamii nchini, Mapitio ya Kanuni za Malezi ya Kambo na Kuasili za Sheria ya Mtoto Sura ya 13, uandaaji wa taarifa ya Ustawi wa Jamii kwenda Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

 

Michango mingine ni mapitio ya Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Makao ya Watoto nchini wa mwaka 2006, kuwezesha Kamati ya kitaifa ya kushughulikia changamoto za  watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani iliyoongozwa vema na Mzee David Mulongo na kusaidia kwa kiwango kikubwa kuwaondoa na kuwapatia huduma watoto hao.

 

 

Kwa upande wake, Rais wa SOS Duniani, Dr. Dereje Wordofa aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipa ushirikiano taasisi yake huku akisema watoto wengi duniani wanakosa huduma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutengana, vita, umasikini na familia kutokuwekeza katika malezi na makuzi ya watoto.

 

 

Kutokana na changamoto hizo alisema jitihada za kuwawezesha watoto katika nchi za Afrika kupata huduma za maji safi ya kunywa na mahitaji yao mengine inakuwa ni ngumu kutokana na mapigano, njaa, ukame na majanga mengine. 

 

 

Naye Kamishna wa Utawi wa jamii nchini Tanzania Dr. Anandela Mhando alisema SOS Children’s Village imekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Kitanzania kwani limeanzisha vijiji vya kutunza watoto wasiokuwa na wazazi ama walezi kwa kuwapatia huduma za elimu na afya.

 

 

“Shirika la SOS Children’s Village wamekuwa msaada mkubwa kwa Wizara ya Maenedeleo ya Jamii, Jinsia na Watu wa Makundi Maalum hasa kwenye afua za kuwafikia watoto ambao wako kwenye mazingira magumu wakiwemo wale watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani, tunafanyanao kazi kupitia kituo chetu cha Kurasini.

 

 

“Lakini pia shirika hili tunafanyanao kazi katika miradi  mingine ya vijana, maendeleo ya jamii, kuwezesha vikundi vya wanawake na vijana na faida wanazozipata zinarudi kusaidia jamii hasa watoto wasiokuwa na wazazi au waliotelekezwa kwa kuwapatia vifaa vya mashuleni.”alisema Dk. Mhando.


No comments:

Post a Comment

Pages