HABARI MSETO (HEADER)


October 23, 2023

ASKARI POLISI WATAKIWA KUIMARISHA MALEZI YA FAMILIA ZAO

Na Issa Mwadangala

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limewaonya askari wenye ndoa wanapozaa watoto kuacha tabia ya kuwapeleka kwa bibi na babu wakalelewe huko,  kwa  kuwa kufanya hivyo husababisha malalamiko, huku wengi wao kukosa huduma muhimu na uangalizi wa karibu zaidi.
Angalizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya,wakati akito nasaha zake  alipohudhuria ibada ya misa ya ndoa ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Antony Sabasaba,  ambaye  ni Msaidizi wa Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Momba.

Tukio hilo la Sakramenti ya ndoa takatifu lilifanyika 
katika kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Parokia ya Mtakatifu Patrick Mjini Vwawa, wilayani Mbozi.

"Kuna 'statement' nimesikia umesema hapo padre kuwa  wanandoa  wawe tayari kupokea watoto na kuwalea, huo ni wosia muhimu  sana kwani tunapata kesi nyingi sana za askari kupeleka watoto kwa wazazi wao na kuwatelekeza bila matunzo".
" Yaani mzazi amekuzaa, amekulea na kukusomesha hadi umepata kazi  kisha unafunga ndoa na unazaa halafu unampelekea  mtoto akulele... hapa hilo halikubaliki na  mimi nitalisimamia na kuchukua hatua" alitahadharisha Kamanda Mallya.

Pia, amewataka askari kuwa mfano bora kwenye jamii kwa kuimarisha malezi ya familia zao ili kuwa na  familia zenye kuchukia uharifu.

 Aidha, Kamanda Mallya ameiasa jamaii kuwa na utaratibu wa kuwa karibu na familia zao ili kuimarisha malezi ya watoto hali ambayo itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto na kuwaepusha kujiingiza kwenye uharifu.

 

No comments:

Post a Comment

Pages