Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Jumuiya
ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Kamati ya
Mshikamano wa Tanzania na Palestina wameziomba na kuzitaka Umoja wa
Mataifa (UN) na Jumuiya za Kimataifa zihakikishe usitishwaji wa vita
kati ya Israel na Plestina.
Akizungumza
na wanahabari jijini humo Mwenyekiti wa JMAT Taifa Sheikh Dkt. Alhad
Mussa Salum amesema kadhia ya vita ya Israel na Palestina imekuwa ni
kadhia ya muda mrefu Mashariki ya Kati kwamba Dunia imeshuhudia mara
kadhaa umwagikaji wa damu kwa pande zote mbili.
"Hata
hivyo kwa upande wa Palestina tumeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za
binadamu dhidi yao. Yanayotokea hivi sasa katika ardhi ya Palestina ni
uvunjifu wa haki za Binadamu na Uvunjifu wa sheria za kimataifa, kama
kupiga mabomu nyumba za Ibada, kupiga mabomu hospitali na vituo vya
afya, kupiga makazi ya raia na hatimaye kuua raia wasio na hatia hasa
wanawake na watoto na kupiga na kuharibu huduma za msingi za kibinadamu
kama maji na umeme," amesema Sheikh Dkt. Alhad Mussa na kuongeza,
"
Jambo hili limetuhuzunisha sana kama wapenda Amani duniani, pia
ifahamike kwa jamii kwamba hivi si vita vya kidini moja kwa moja na
visitugawe kati ya Waislam na Wakristo na watu wa dini nyingine
mbalimbali. Aidha wanaouawa ni pale ni Waislam, Wakristo, pengine na
wasiokuwa na dini,".
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa JMAT Taifa Askofu Dkt. Israel Ole-Gabriel
Maasa amesema mambo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kwa watu
wastaarabu.
Kwamba dini za Ukristo na Uislam pamoja na dini nyingine zote kwa ujumla hazikubaliani na uharibufu wa namna hiyo.
"Hivyo
basi, tunaziomba na kuzitaka mamlaka husika hasa Umoja wa Mataifa na
Jumuiya za Kimataifa zihakikishe usitishwaji wa vita hivyo mara moja
pamoja na kuhakikisha huduma za kibinadamu hasa maji, umeme, dawa na
huduma nyingine zinarejeshwa mara moja," ameeleza Askofu Dkt. Maasa.
Kadhalika
ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuangalia kiini cha tatizo hilo na hivyo
kupata ufumbuzi wa kudumu na amewaomba pia wadau na wapenda amani wote
duniani kuzidi kupaza sauti zao dhidi ya uhalifu huu wa Kivita Mashariki
ya Kati.
No comments:
Post a Comment