Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akihutubia katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Wakandarasi waliowekeza kwenye Madini yanayopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu unaofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijjini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22 hadi 24 Oktoba, 2023 ambapo utafungwa rasmi tarehe 24 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
Na Wizara ya Madini, Dar es Salaam
Serikali
ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini kwa mara nyingine imeweka Historia
ya kuwa Nchi ya Kwanza Barani Afrika kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Sita
(6) wa Kimataifa wa Wakandarasi waliowekeza kwenye Madini yanayopatikana
Chini ya Sakafu ya Bahari Kuu ambapo nchi inapata fursa ya kujifunza
kuhusu utafiti, uvunaji na uendelezaji wa rasilimali hiyo.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati wa
ufunguzi wa Mkutano huo wa Siku Tatu ulioanza leo tarehe Oktoba 22, 2023
jijini Dar es Salaam na utaendelea hadi Oktoba 24, 2023 huku
ukitarajiwa kufungwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Kassim Majaliwa.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Kiruswa amesema umelenga
kuwafahamisha washiriki kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika
maandalizi ya kuandaa Kanuni zitakazotoa mwongozo wa namna dunia
itakavyonufaika na uvunaji wa rasilimali hiyo inayopatikana katika
sakafu iliyo chini ya bahari kuu.
Ameongeza
kwamba, pamoja na mambo mengine mkutano huo unatarajia kujadili ajenda
mbalimbali kuhusu masuala ya utafiti, uchimbaji, utunzaji wa mazingira
yaliyo chini ya sakafu ya bahari kuu ikiwa ni kuendelea na utekelezaji
wa Article 145 ya UNCLOS Umoja wa Mataifa na makubaliano ya mwaka 1994
kuhusu shughuli za uchimbaji wa madini kwenye sakafu ya bahari.
‘’Nchi
wanachama wa umoja wa Mataifa zinaandaa kanuni zitakazosimamia uvunaji
wa rasilimali hizo kutokana na nchi nyingi duniani kuwa na wasiwasi
kuhusu madhara ya kimazingira yanayoweza kusababishwa na shughuli za
uchimbaji wa madini haya. ‘’ Kimsingi uchimbaji wa madini haya hauwezi
kuharibu mazingira ya bahari bali madini haya yanachotwa kwa kutumia
kifaa kiitwacho “collector” tu na kuletwa juu ya ardhi,’’ amefafanua
Dkt. Kiruswa.
Akizungumza
ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ikiwa ni miongoni mwa nchi
wanachama wa umoja huo amesema ni nafasi kwa Tanzania kuendelea
kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu rasilimali madini iliyo chini ya
sakafu ya bahari ikiwemo kutafiti, kuvuna na kuiendeleza ili kunufaika
ipasavyo na rasilimali hiyo ikiwa ni moja ya maeneo muhimu wa Uchumi wa
Buluu.
Ameongeza kwamba,
huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuendeleza rasilimali
madini hususan madini muhimu na mkakati na kwa kuzingatia *Vision 2030:
Madini ni Maisha na Utajiri* ambayo inalenga kufanya utafiti wa kina kwa
kutumia ndege angalau kufikia asilimia 50 ya eneo zima la nchi ifikapo
mwaka 2030 ili hatimaye madini hayo yaweze kuongeza tija zaidi katika
uchumi na mchango wa sekta ya Madini katika maendeleo ya nchi.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kimataifa ya
Usimamizi wa Madini yanayopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu
(International Seabed Authority – ISA) Dkt. Marie Bourrel- MacKinnon
ameipongeza Tanzania kuonesha dhamira ya uendelezaji wa madini hayo na
kusema kwamba ushiriki wake katika mkutano huo utaisaidia kufanya
maamuzi sahihi juu ya matarajio yake ya baadaye. Pia, ameongeza kuwa,
mikutano kama hiyo inatoa fursa ya muhimu ya wanachama kujadili kwa kina
na kutafakari namna bora zitakazowezesha kutoa uwiano sahihi na wa
kutosha kwa maslahi ya wote.
Amesisitiza
kuwa, wakandarasi hao wa madini yaliyo chini ya sakafu ya bahari kuu
wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni zinazoongoza katika
hatua mbalimbali za utafutaji wa madini hayo.
Awali,
akizungumza katika ufunguzi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini
Msafiri Mbibo amesema Tanzania bado haina ujuzi na teknolojia za
kutafiti na kuchimba madini yaliyochini ya sakafu ya bahari kuu hivyo,
ushiriki wake na uwenyeji wake katika mkutano huo utaisaidia kujifunza,
kupata ujuzi na kujengewa uelewa wa namna ya kuendeleza madini hayo.
Aidha,
ameeleza kuwa, mkutano huo ni wa manufaa kwa Tanzania kwa kuwa
utaiwezesha kujenga na kuimarisha mahusiano yatakayoisaidia kuendeleza
rasilimali hiyo.
Kwa
upande wa Tanzania, mbali na ushiriki wa viongozi na wataalam kutoka
Wizara, Taasisi zake, pamoja na taasisi nyingine za umma, pia,
umehudhuriwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Serikali kwenye Umoja wa
Tanzania , Mhe. Balozi Hussein Kattanga.
Tanzania
inashiriki ikiwa ni miongoni mwa nchi 169 wanachama wa Mamlaka ya
Kimataifa ya Usimamizi wa Madini hayo (ISA) ambayo iko chini ya Umoja wa
Mataifa yenye makao makuu yake Kingston nchini Jamaika.
Mkutano
wa Sita umeshirikisha watu binafsi, na wawakilishi kutoka wakandarasi
15 huku wengine 16 wakishiriki kwa njia ya mtandao.
Mkutano
huo hufanyika kila mwaka ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa shughuli
zote za utafiti, uchimbaji na utunzaji wa mazingira yazingatiwa. Hadi
kufikia sasa kuna wakandarasi wapatao 31 wa nchi zinazodhamini kutoka
Ulaya, Amerika, Asia na Karibian ambazo zinaendela kutekeleza shughuli
za utafiti wa madini aina ya Polymetalic Manganese Nodules (PMN),
Sulphide na madini mengine yanayopatikana chini ya sakafu ya bahari
ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa teknolojia za kisasa.
Aidha,
mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu isemayo *Kuimarisha mahusiano na
uwajibikaji katika usimamizi warasilimali za madini yaliyopo chini ya
sakafu ya bahari kuu*
No comments:
Post a Comment