HABARI MSETO (HEADER)


October 23, 2023

WATATOANA NYONGO DAR DERBY

NA JOHN MARWA


NI leo pale Benjamin Mkapa ambapo mchezo wa haja utawakutanisha Mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Matajiri wa Chamazi, Azam FC, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC PL) utaoalindima kuanzia majira ya saa 12:30 jioni kwa saa za afrika mashariki.


Ni mchezo wa aina yake pale Lupaso kwani timu itakayofanikiwa kuibuka na alama tatu itakwea hadi kwenye kilele cha msimamo na kuwashusha Simba SC kwa muda wakiwa na majukumu ya kimataifa ya Ligi ya Kandanda Barani Afrika AFL.

Yanga ikiibuka na  itafikisha pointi 15 sambamba na Simba ingawa zitatofautiana zaidi kwenye michezo na mabao ya kufunga na kufungwa. 


Azam ambayo haijapoteza mchezo kati ya mitano iliyocheza, ikishinda itafikisha pointi 16 na kukwea kileleni jambo ambalo linaongeza ushindani mkali kwa miamba hii wakati itakapokuwa inapambana jioni ya leo.


Mchezo wa leo ni wa 31 kwa timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu Azam FC ilipopanda rasmi Julai 27, 2008, baada ya kuifunga Majimaji ya Songea mabao 2-0, Uwanja wa Jamhuri Dodoma na Yanga imeshinda 12, sare tisa na kupoteza tisa.

KAULI ZA MAKOCHA
Wakizungumza kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo alisema Yanga ni timu bora ambayo wanaiheshimu kwa kiasi kikubwa ila wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza rekodi  nzuri ya kutopoteza mchezo wowote wa ligi.

“Sio rahisi unapocheza na timu kama Yanga kwa sababu ina wachezaji wazuri ambao tayari wameonyesha ubora mkubwa msimu huu, hivyo kwetu ni kipimo sahihi cha kuonyesha ni kwa jinsi gani tunahitaji kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema licha ya kuwaheshimu wapinzani wao kutokana na ubora waliokuwa nao msimu huu lakini malengo yao makubwa ni kupata pointi tatu ambazo zitazidi kuwatengenezea mazingira mazuri mbeleni.

No comments:

Post a Comment

Pages