“Sisi wawekezaji tumefurahi na kuridhishwa na ufanisi katika uendeshaji wa kiwanda hiki cha sukari cha TPC Limited, ufanisi huu unatoka na faida iliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2022/23 ambapo kiwanda kimeweza kuzalisha faida baada ya kodi ya shilingi 72.7. bilioni kutoka katika mauzo ya shilingi bilion 235 huku gawio kwa wanahisa ikiwa ni shilingi bilioni 69.9” hayo yamesemwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu baada ya kikao cha wanahisa kilichofanyika jana mkoani Kilimanjaro.
Mchechu
anasema tangu mwaka 2000 kiwanda hiki kimekuwa kikiongeza uzalishaji
mwaka hadi mwaka ambapo kwa sasa uzalishaji wa sukari umeongezeka kutoka
Tani 36,000 za mwaka 2000 hadi kufikia Tani 116,700 kwa mwaka huu.
Mchechu
anaeleza ongezeko hilo la uzalishaji wa sukari limetokana na ongezeko
la mavuno ya miwa ambapo kwa mwaka huu kiwanda kimevuna miwa zaidi ya
Tani 1,150,000.
“Katika uzalishaji wa sukari kwa mwaka huu, TPC
Limited imezalisha zaidi ya tani 116,700 katika kipindi cha juni 2022
hadi machi 2023, hiki ni kiwango kikubwa sana cha sukari ambacho
hakijawahi kuzalishwa katika miaka yote tangu TPC Limited kuanza
uzalishaji wake mwaka 1936”.
Anasema wakati wanafanya
ubinafsishaji wa kiwanda hicho, serikali ilikuwa imeweka malengo shamba
la TPC baada ya kuwa imeongezewa eneo la shamba la Kahe, itaweza
kuzalisha tani 750,000 kwa mwaka, lakini kwa sasa wanazalisha Tani
1,150,000 ambayo ni juu ya malengo waliyokuwa wamewekwa na serikali
wakati wa ubinafsishaji.
“Eneo lile lile lakini uzalishaji
unazidi kuwa mkubwa kutokana na tija katika uzalishaji kwani kwa mwaka
huu TPC tumeweza kutoa tija ya wastani wa tani 148 (tani mia moja na
arobaini na nane) kwa hekta kiwango ambacho ni cha juu barani Afrika,
na ni moja kati ya viwango bora vitatu duniani” anasisitiza Mchechu.
Akizungumzia
sababu ya ufanisi na mafanikio hayo, Mchechu anasema Serikali ya awamu
ya sita imeweka nguvu na jitihada kubwa za kuhamasisha kilimo na kuvutia
uwekezaji katika kilimo hususani katika sekta ya sukari na hilo
limeweza kufungua fursa nyingi kwenye sekta ya sukari nchini.
Anasema
mambo ambayo yamefanyika katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita
ni pamoja na kuendelea kulinda soko la ndani dhidi ya sukari
zinazoingizwa zenye kiwango cha chini na kuja kushindana na sukari
inayozalishwa nchini yenye kiwango bora.
Anaeleza kuwa kitendo
hicho kimefanya sukari kuendelea kuuzwa katika bei nzuri na hivyo
kuhamasisha wazalishaji wa sukari kuendelea kuwekeza zaidi katika soko
la sukari.
“Tumeshuhudia serikali imekuwa na mfumo unaoeleweka na
endelevu wa uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi na hii ni kutokana na
maboresho yaliyofanyika katika sheria ya sukari pamoja na kanuni zake
ambapo uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi, umewekewa utaratibu mzuri
zaidi”.
Anasema eneo lingine ambalo serikali imefanya ni
kuhamasisha na kuhakikishia wawekezaji mazingira mazuri ya uwekezaji
hali ambayo imechangia kupanda kwa idadi ya wekezaji kutoka ndani na nje
ya nchi wanaowekeza katika sekta ya sukari.
“Vipo viwanda mbavyo
vimeanza kufanya kazi lakini pia kuna viwanda vingine vinakuja kuweza
kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, hivyo katika mazingira haya
tumeona serikali ya awamu ya sita, imesukuma mbele jitihada za kukuza
kilimo hususani cha miwa, ili kuongeza uzalishaji wa sukari hapa
nchini”.
Anasema katika kuunga mkono jitihada hizo za serikali,
TPC kwa mwaka huu wanatazamia kuwekeza fedha Dola 45 milioni hadi 50
milioni kwa kujenga kiwanda kipya cha kuchakata Molasses ambayo imekuwa
ikibaki baada ya uzalishaji wa sukari.
“Bodi yetu leo
itaidhinisha matumizi ya fedha zaidi ya Dola 45 milioni ama Dola 50
milioni kwa ajili kuweka kiwanda kingine cha uchakataji Molasses na
kuweza kuzalisha bidhaa nyingine ambayo itakuwa ni spirit kwa ajili ya
matumizi ya viwanda na watumiaji wengine".Anasema kiwanda hicho
kitajengwa TPC na ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema 2024, na kwamba
hicho ni kiwango kikubwa cha fedha kitakachowekezwa ambapo ni pamoja na
kukuza zao la miwa na bidhaa zinazotokana na zao la miwa.
Anaeleza
kuwa uwekezaji huo kwa TPC utakuza ajira pamoja na kuongeza mapato ya
ndani ya kiwanda na kuwezesha kulipa kodi nyingi zaidi na manufaa
mengine yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo.
Anasema kubwa
zaidi kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa nishati ya umeme ambapo
katika kiwanda hicho wanatarajia kufunga mashine nyingine ya kuzalisha
umeme na hivyo kutakuwa na ziada ya megawati Nne hadi saba ambazo
zitaingizwa katika gridi ya Taifa.
Akizungumzia mchango wa
Kiwanda cha Sukari cha TPC kwa jamii, Jafarry Ally ambae ni Mkuu wa
Utawala katika kiwanda hicho anasema TPC imeweza kulipa kodi, ushuru
pamoja na gawio kwa serikali zaidi ya Sh. 99 bilioni, kiwango ambacho ni
kikubwa ukilinganisha na kiwango cha Sh. 2 bilioni kilichokuwa
kikitolewa wakati kampuni hiyo imebinafsishwa mwaka 2000 na sababu kubwa
ya kuongezeka kwa kiwango hicho ni uzalishaji,mauzo mazuri na ulipaji
sahihi wa kodi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya ulipaji kodi.
“Mwaka
2010 ndipo kiwanda kilianza kulipa gawio serikali na hadi mwaka
2022/2023 tumekuwa tukilipa gawio na kiwango kimekuwa kikiongezeka mwaka
hadi mwaka na kuifanya TPC kuongoza kwa miaka mitatu mfululizo kwa
kutoa gawio zuri na kubwa serikalini kuliko mashirika mengine yote
ambayo serikali ina hisa kidogo”.
Akizungumzia mchango wa kiwanda
hicho kwa jamii Ally anasema kwa kupitia shirika lao lisilo la
kiserikali la FTK, wamekuwa wakitumia Sh1.2bilioni kwa mwaka kwa ajili
ya kuhudumia jamii ya vijiji vinavyowazunguka ambapo fedha hiyo
inaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu,
afya, miundombinu na miradi endelevu ya vijiji kama miradi ya
umwagiliaji.
“Kwa upande wa utoaji wa huduma katika vijiji
vinavyotuzunguka tumeendelea kuboresha huduma na kwa upande wa elimu,
hivi karibuni tumejenga shule ya sekondari ya Chekereni/Weruweru(CHEWE)
ambayo ni ya serikali, na serikali ilituletea fedha za uviko ikaja
kuongezea majengo ambayo imefanya shule hiyo kuwa na vitu vingi
vilivyokamilika.”
“Ni shule inayoanza lakini ina vitu vyote
muhimu ikiwemo madarasa, vyoo, jiko, madawati, maabara zote pamoja na
jengo la utawala na shule hii itazinduliwa hivi karibuni baada ya
serikali kukamilisha uwekaji wa samani”
“Lakini pia tumeweza
kutoa huduma za afya na kujenga mundombinu ya barabara kutokana na uwezo
tunaokuwa nao ikiwa ni pamojana kuchimba visima na kujenga mabwawa ya
kuoshea mifugo katika vijiji vinavyotuzunguka”.
No comments:
Post a Comment