Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) imefuta na kupunguza jumla ya tozo, ada na faini zisizopungua 232 kati ya 380 zilizobainishwa katika utekelezaji wake sawa na asilimia 61.
Akizungumza Kikao Maalum cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, Dkt Jim James Yonazi alisema ufutwaji wa tozo, ada na faini hizo ambazo zilikuwa kero kubwa kwa ustawi, ukuaji na maendeleo ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
“Maamuzi haya yanaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifungua Tanzania na kuwa kivutio cha kufanya biashara na uwekezaji,” alisema Dkt. Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi kazi hicho cha Baraza la Taifa la Biashara(TNBC).
Akielezea zaidi mafanikio yaliyopatikana tangu MKUMBI uanze kutekelezwa, Dkt. Yonazi alisema jumla ya Sheria, Kanuni na Taratibu zipatazo 40 kati ya 88 sawa na asilimia 45.5 zimeshapitiwa na kufanyiwa marekebisho.
“Maboresho haya yote ya Sheria,Kanuni na Taratibu yamesaidia kuchochea ukuaji wa sekta za uchumi hapa nchini zikiwemo sekta za uwekezaji, viwanda na biashara, kilimo, mifugo, afya, maliasili na utalii,” alisema.
Dkt. Yonazi alisema Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC ameelekeza kuendelea kusimamia utekelezaji stahiki wa MKUMBI sambamba na uhamasishaji wa matumizi ya mifumo yaTeknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini.
“Nina agiza Wakurugenzi na Idara za Uratibu, Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Maendeleo ya Sekta Binafsi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,wafuatilie utekelezaji wa Maazimio ya TNBC na kuwaandikia barua Makatibu Wakuu wote ambao bado hawajawakilisha taarifa za utekelezaji wa maazimio hayo,” alisisitiza Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi alimpokeza Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga na watendaji pamoja na wafanyakazi wote wa baraza kwa kazi nzuri na kuwakumbusha wajumbe wote kwenye Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara kuendelea kufanyia kazi maono na matarajio ya Rais Hassan.
Kwa upande wake, Dkt. Wanga alisema Kikosi Kazi cha Mazingira ya Biashara kina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mazingira ya kufanya biashara yanaendelea kuwa rafiki kwa biashara, uwekezaji na uchumi kwa ujumla na kuvutia uwekezaji kujenga uchumi wan chi.
“Kikundi kazi hiki kina jukumu kubwa la kuondoa na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji. Hivi hatuna budi kufanya kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunaandaa na kuwakilisha mapendcekezo yenye tija kwa Baraza,” alisema Dkt. Wanga.
Alisema TNBC hufanya kazi kupitia mikutano na vikao katika ngazi mbalimbali kama vile ya Baraza,Kamati Tendaji za Baraza, Mashauriano ya Kiwizara kati ya Sekta Binafsi na Umma(MPPD), Kikosi Kazi cha Kiufundi cha Kiwizara(MTWG), Mikutano ya Baraza la Biashara ngazi ya Mkoa (RBC) na Wilaya (DBC).
No comments:
Post a Comment