WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema watoa huduma za kifedha hawana budi kujenga uelewa wa
kutosha kwa wananchi kabla ya kufunga nao mikataba, pamoja na
kuwafafanulia taratibu na masharti yao kabla hawajatoa kwao huduma hizo
za fedha.
Pia amewataka watoa huduma hao waweke mkakati mahususi wa
kuongeza matumizi huduma kwa njia ya kidijitali pamoja na kuzisogeza
hadi maeneo ya pembezoni na vijijini ili wananchi walio wengi wanufaike.
“Watoa
huduma za fedha ongezeni ubunifu katika utoaji wa huduma. Toeni huduma
zinazoendana na wakati, mahitaji ya soko na kuzingatia uhitaji wa
makundi mbalimbali katika jamii. Suala hili liende sambamba na
kuwaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta ya
fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao. "
Amesema
lengo la maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa na Maonesho ya
Huduma za Fedha yamejikita katika kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu
matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa, kusimamia vizuri
rasilimali fedha ikiwa ni pamoja na kuimarisha utamaduni wa kujiwekea
akiba, kukopa kutoka vyanzo salama na njia sahihi za kulipa madeni ili
kujenga uchumi na kuondoa umaskini.
Naye,
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea
kukuza uelewa kwa Watanzania kuhusu masuala ya kifedha huku akitoa wito
kwa Watanzania kuweka utaratibu wa kusoma vigezo na masharti ya huduma
za kifedha wanazopata kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha ili
kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadae.
Kwa
Upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bi. Natu El-maamry amesema
maadhimisho hayo ya tatu ni muendelezo wa jitihada za Serikali katika
kuongeza uelewa wa masuala fedha kwa Watanzania ili waweze kuwa na
uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za kifedha.
Afisa Masoko na Uhusiano wa Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Martha Mashiku (wa pili kulia), akitoa elimu ya uwekezaji wa pamoja kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa kwa Wizara ya Fedha kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
Afisa
Masoko na Uhusiano wa Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Martha Mashiku (kulia),
akiwa na Afisa wa UTT kutoka Mkoa wa Arusha katika Wiki ya
Huduma ya Fedha Kitaifa, jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment