HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 29, 2023

Mbunge Kyombo apongeza juhudi za wana Bwanjai ahaidi ushirikiano

Mbunge wa Jimbo la Nkenge Wilayani Misenyi Mkoani Kagera na Makamu Mwenyekiti wa kamati  ya kudumu ya Bunge ya utawala, Katiba na sheria Florent Kyombo amepongeza juhudi za wana Bwanjai zinazoonyesha maendeleo ya haraka na ya muda mfupi katika kata ya Bwanjai Wilayani humo.


Kyombo alitoa pongeza hizo baada ya kuona hatua kubwa ya maendeleo na mafanikio yaliyopatikana  kutokana na umoja huo wa Jumuiya ya Bwanjai (BWANJAI COMMUNITY ASSOCIATION) - BCA wakati akiwa Mgeni rasmi katika siku ya Bwanjai maarufu BWANJAI DAY ambayo hufanyika Desemba 27 ya kila mwaka.


Mbunge huyo amesema tangu kuanzishwa kwa Bwanjai Day 2015 wamepiga hatua za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha baadhi ya Barabara za vitongoji kwa kuweka vifusi, kuwepo mfuko wa Elimu uliosaidia kuwalipia Wanafunzi wasiokuwa na uwezo na kusomeshwa, ununuzi wa matenki mawili ya maji lita 5, 000 sawa na lita 7,000 katika shule ya Sekondari Bwanjai, utengenezaji wa madawati 162 viti 81 kupitia Bwanjai Day.


"Niwapongeze Wanabwanjai waishio ndani ya kata na nje ya kata ambao mmeonyesha ushirikiano na umoja hadi kufanikiwa haya niwaombe muendelee kushirikiana ili Bwanjai iwe ya mfano alisema Mbunge Kyombo".


Aidha aliahidi kuhakikisha anatoa ushirikiano wa kutosha na kukamilisha baadhi ya ahadi na kuwaomba Wanabwanjai kujikita katika vipaumbele ambavyo wamejipangia huku akisema fedha zinazotakiwa kutoka mfuko wa Jimbo ambazo ni shilingi Bilioni 7 zitawafikia ili kujenga Zahanati na nyingine kuongezwa kwenye umaliziaji wa Bweni la wasichana huku akiongeza kuwa atakaa Madiwani wa kata ya Bwanjai Phocus Rwegasira kama Baraza la Madiwani ili wahakikishe wanaingiza suala hilo kwenye bajeti na mwaka ujao wapate meza na viti.


Aidha akisoma Risala mbele ya Mgeni rasmi katibu wa BWANJAI COMMUNITY ASSOCIATION Mwl. Placidius  France alisema kuwa Viongozi na Wananchi waishio ndani na nje ya kata hiyo kwa ujumla walikaa kwa pamoja, kwa kushirikiana na kamati  ya maendeleo ya kata ambapo walibaini changamoto zilizopo katika maeneo yao na kuanzisha umoja huo ili kuzipatia ufumbuzi.


France amesema baada ya kuanzisha umoja huo waliweka vipaumbele vya kata ambavyo ni ujenzi wa Bweni la  wasichana shule ya Sekondari Bwanjai, ujenzi wa Ofisi ya kata, kuboresha vyanzo vya utalii vilivyopo, kujenga jengo la utawala Bwanjai Sekondari.


Katibu huyo alimuomba mbunge wa Jimbo la Nkenge Florent Kyombo kuwezesha mradi wa Bweni la wasichana shule ya Sekondari Bwanjai kukamilika haraka baada ya mradi huo kusuasua kwa michango ambayo inatolewa na kusababisha ujenzi wa mradi huo kutumia muda mrefu bila kukamilika.


Hata hivyo naye Diwani wa kata ya Bwanjai Phocus Rwegasira amesema kuwa kata hiyo imepiga hatua kubwa kutokana na ushirikiano wa Wanabwanjai na kuwa awali walikuwa hawana Katiba wala uongozi Ila sasa wamesajiliwa huku lengo lao kubwa likiwa ni kutoisubiri Serikali katika shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages